Petroli na mafuta ya taa bei juu

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta ya petroli na mafuta ya taa nchini watalazimika kutumia fedha zaidi kupata lita moja ya mafuta baada ya bei kuongezeka, wakati watumiaji wa dizeli wakipata ahueni.

Hiyo ni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia Jumatano, Januari 7, 2026 saa 6:01 usiku.

Wakati ongezeko na kushuka kwa bei kukishuhudiwa nchini, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 4.26 kwa mafuta ya petroli, asilimia 12.83 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 10.44 kwa mafuta ya taa.

Bei hiyo imepungua pia wakati ambao gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.1 kwa mafuta ya petroli, asilimia 4.0 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.

Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la gharama hizo katika Bandari ya Tanga, ambapo zimeongezeka kwa asilimia 3.5 kwa petroli na dizeli na katika Bandari ya Mtwara zimeongezeka kwa asilimia 11.5 kwa mafuta ya petroli, huku kukiwa hakuna mabadiliko kwa mafuta ya dizeli.

Kufuatia hilo, sasa kwa mujibu wa taarifa ya Ewura iliyotolewa, wanunuzi wa lita moja ya petroli inayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam watatumia Sh2,778 kwa lita Januari mwaka huu kutoka Sh2,749 waliyokuwa wakitumia Desemba mwaka jana.

Wakati huohuo, watumiaji wa dizeli watapata ahueni, kwani lita moja watanunua kwa Sh2,726 kutoka Sh2,779 waliyotumia Desemba mwaka jana, wakati mafuta ya taa yakiongezeka hadi Sh2,763 kutoka Sh2,653.

Kwa watumiaji wa mafuta yanayopita katika Bandari ya Tanga, watanunua petroli kwa Sh2,839 Januari mwaka huu kutoka Sh2,811 waliyonunua Desemba mwaka jana, huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh2,787 kutoka Sh2,766 na mafuta ya taa kwa Sh2,856 kutoka Sh2,714, mtawalia.

Kwa wale wanaochukua mafuta kupitia Bandari ya Mtwara, watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,870 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2,842 iliyokuwapo Desemba mwaka jana, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,818 pungufu kutoka Sh2,872 na mafuta ya taa yakifika Sh2,856 kutoka Sh2,745, mtawalia.

Taarifa hiyo ya Ewura inaeleza kuwa kwa bei za Januari 2026, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umeongezeka kwa asilimia 1.31.

Kufuatia hilo, Ewura imewataka wafanyabiashara kuuza mafuta kwa bei zilizotajwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.

“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana, yakionesha bei za mafuta, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kuhamasisha ushindani,” imeelezwa.

Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei yanayoonekana vizuri kwa wateja, na adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

“Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” imeelezwa.

Stakabadhi hizo zitatumika kama ushahidi kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.