Saba kortini wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya

Dar es Salaam. Mkazi wa Sinza Kijiweni, jijini Dar es Salaam, Cuthbert Kalokola (34) na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa mashtaka saba ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, Flunitrazepan na bangi.

Mbali na Kalokola, washtakiwa wengine ni Mulhath Abdallah(19) mkazi wa Chamazi; Fredrick Jesca(26) mkazi wa Ubungo; Alphonce Baracka(25) mkazi wa Ubungo Tanesco; Glory Miala(23) mkazi wa Ubungo Darajani; Frank Joachim(25) mkazi wa Namanga Tegeta pamoja na Emmanuel Mapala(25)mkazi wa Ubungo.

Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakama hapo leo Jumatano, Januari 7, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali Christopher Olembille.

Wakili Olembille aliwasomea mashtaka yao, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.

Olembille alidai shtaka la kwanza ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi linalomkabili Kalokola na Abdallah.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 15, 2025 eneo la Sinza D, Wilaya ya Ubungo, washtakiwa waliongoza genge la uhalifu kwa kukutwa na dawa za kulevya.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Shtaka la pili, Kalokola na Abdallah wanadaiwa Novemba 15, 2025 eneo la Sinza D, walikutwa wakisafirisha gramu 2160.05 za bangi.

Shtaka la tatu ni kwa mshtakiwa Kalokola na Abdallah wanadaiwa walisafiirsha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa gramu 944.47.

Vile vile, Kalokola na Abdallah wanadaiwa tarehe hiyo na eneo hilo, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Flunitrazepan zenye uzito wa gramu 10.03.

Wakili Olembille alidai shtaka la tano ni kwa ajili ya mshtakiwa wa Jesca pekee yake, ambapo Novemba 15, 2025 eneo la Ubungo Kibo, alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 42.93.

Shtaka la sita ni kwa ajili ya mshtakiwa Miala, Joachim na Mapala, ambao Novemba 15, 2025 eneo la Ubungo Kibo karibu na Tanesco,  wanadaiwa kusafirisha gramu 116.12 za bangi.

Shtaka la saba linamkabili Mapala, Novemba 14, 2025 eneo la Uhasibu alikutwa na gramu 24 za bangi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, wakaomba Mahakama ipange tarehe nyingine.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo waliomba wapewe dhamana.

Mshtakiwa Kalokola anatetewa Nashoni Nkungu na mshtakiwa Abdallah yeye anatetewa na Wakili Hassan Chande.

Kwa upande wa mshtakiwa wa tatu hadi wa saba, wao hawana wakili anayewatetea, hivyo wanajitetea wenyewe.

Hakimu Mbuya alisema mshtakiwa Kalokola na Abdallah wao hawana dhamana kutoka na dawa walizoshtakiwa nazo hazina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Pia, hakimu Mbuya alisema kuanzia mshtakiwa wa tatu hadi wa saba, mashtaka yao yanadhaminika na kisha kutoa masharti ya dhamana.

Hakimu Mbuya alitoa masharti manne, ambayo ni kila mshtakiwa anatakiwa awasilishe fedha taslimi Sh5milioni au mali iaiyohamishika yenye thamani hiyo.

Vile vile washtakiwa hao wanne, wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za mitaa na watasaini bondi ya Sh10milioni.

Vile vile wanatakiwa kukabidhi Mahakama hati zao za kusafiria kama wanazo.

“Washtakiwa wanne, hamtakiwi kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama,” alisema Hakimu Mbuya.

Hata hivyo, washtakiwa hao wanne wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kurudishwa rumande.

Kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo, Januari 22, 2026.