Mufindi. Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) – Afya, Dk Jafari Rajabu Seif, amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zote ndogo ndogo zinazojitokeza katika Hospitali ya Mji Mafinga.
Kauli hiyo ameitoa Januari 7, 2026, wakati akifanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu katika Hospitali ya Mji Mafinga pamoja na Kituo cha Afya Upendo.
Dk Seif amebainisha kuwa kutokana na unyeti na mahitaji ya kipekee ya huduma katika hospitali hiyo, Serikali itahakikisha changamoto zote zinatatuliwa ili wananchi wapate huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
Aidha, Dk Seif amesema kuwa Serikali imetenga zaidi ya Sh230 milioni, ambazo tayari zimepelekwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Hatua hiyo itawawezesha kuanza kikamilifu utendaji wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) ya Hospitali ya Mji Mafinga, taasisi inayopokea rufaa nyingi kutoka maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na hospitali hiyo.
Mbunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele shukrani amesema hospitali hiyo imepokea Sh900 milioni, fedha ambazo zimewezesha ujenzi wa jengo la ICU pamoja na miradi mingine ya maendeleo, huku changamoto ya upungufu wa watumishi ikishughulikiwa kwa hatua mbalimbali.
Dk Seif pia ametoa rai kwa watumishi wa afya katika hospitali zote za jimbo hilo wenye dhamana ya kuwahudumia wananchi, akiwahimiza kuwa waendeleze bidii hiyo ili sera na dhamira za Serikali ya Awamu ya Sita zifanikishwe kwa vitendo.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawahitaji majengo tu, bali huduma bora zinazotolewa kwenye vituo vya afya, ikizingatiwa mipango ya Serikali inayowaelekeza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Regnant Kivinge, amesema kama madiwani wataendelea kusimamia miradi hiyo kwa uangalifu, itakuwa rahisi kuona thamani halisi ya fedha ambazo Serikali inazitenga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa katika jitihada za kuhakikisha miradi ya afya inakidhi mahitaji ya wananchi kwa ufanisi na uwazi.
“Tunaahidi kumwakilisha vema Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia vizuri uwajibikaji, miradi na ukusanyaji wa mapato tuweze kuwa na miradi mingi yenye tija kwa watu ili wananchi waweze kuona Serikali ipo kazini kwa sababu zamani watu walikuwa wanaamini sana maneno lakini kwa sasa watu wanahitaji vitendo zaidi kuona changamoto wanazokabiliana zinatatuliwa,” amesema Kivinge.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya hospitali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dk Victor Msafiri, amesema kuwa licha ya kukamilika kwa ujenzi wa baadhi ya majengo ya ICU na ‘Theater’, bado hayajatumika kutokana na ukosefu wa vifaatiba muhimu.
Dk Msafiri ameorodhesha baadhi ya vifaa vinavyohitajika kuwa ni pamoja na mashine za usingizi, vitanda vya ICU, mashine za kusaidia kupumua, mashine za kufuatilia maendeleo ya mgonjwa, mashine za kupima umeme wa moyo (ECG), pamoja na mashine ya mionzi inayoweza kusogea.
Vifaa hivi ni muhimu kuhakikisha hospitali hiyo inakidhi mahitaji ya huduma za afya kwa wagonjwa wanaoruhusiwa rufaa kutoka maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na taasisi hiyo.
“Hospitali imeendelea kununua vifaatiba ambavyo vinawezesha huduma kuendelea kutolewa kwa kiasi lakini na mkurugenzi wetu wa halmashauri ya Mji Mafinga ameandika barua ya maombi ya vifaatiba kwa Katibu Tawala mkoani hapa ili majengo haya yaweze kutumika kikamilifu,” amesema Dk Msafiri.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kutokana na uboreshaji huo wa miundombinu utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa mahututi, kupunguza mrundikano wa wagonjwa wodini, kupunguza maambukizi yanayosababishwa na msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma ya mama na mtoto.