Dar es Salaam. Ingawa mara nyingi harusi ni tukio linalofurahiwa na kusherehekewa, hali imekuwa tofauti kwa Zainab Kombo, aliyefanya sherehe baada ya kupewa talaka na aliyekuwa mume wake.
Hatua ya Zainab imeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau wa maadili, wataalamu wa sosholojia, viongozi wa kiroho na Serikali, baadhi wakimuunga mkono, huku wengine wakimpinga.
Wanaomuunga mkono wanasema sherehe hiyo inatoa ujumbe wa furaha ya kujinasua kutoka katika wimbi la maumivu, manyanyaso na uonevu walioupitia ndani ya maisha ya ndoa.
Lakini wanaompinga wanasema, haijalishi umepitia mangapi, kusherehekea talaka kunakitengenezea kizazi kijacho mtazamo wa kukosa subira ya kutatua migogoro ya ndoa na hatimaye kuifanya taasisi hiyo kuwa dhaifu.
Viongozi wa dini wao wanasema sherehe za talaka zinapaswa kupingwa kwa sababu hazitoi mfano mwema kwa jamii na zinavunja heshima iliyopewa taasisi ya ndoa.
Katikati ya mitazamo hiyo, Serikali inaona haja ya kufanyika uchambuzi kujua ilikuwaje sherehe hizo zinatokea, kwa ukubwa gani, malengo yapi, na matokeo chanya na hasi ni yapi na kwa nani.
Tukio la sherehe ya talaka lililopewa jina la ‘Usiku wa Talaka’ lilifanyika Januari 4, mwaka huu, likihudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki na majirani wa Zainab.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari kuhusu sababu za sherehe hiyo, Zainab anasema aliitaka talaka, ndiyo maana amesherehekea baada ya kuipata.
Hata hivyo, hakuweka wazi changamoto za maisha yake ya ndoa, ingawa alieleza matatizo ndani ya ndoa ni siri ya mume na mke.
Mwananchi jana, Jumanne Januari 6, 2025, imezungumza na dada yake Zainab, Aisha Othman, anayesema mdogo wake alishakuwa kwenye ndoa mbili kabla ya tatu, ambayo talaka yake ameifanyia sherehe.
Anasema aliingia kwenye ndoa ya kwanza akioneshwa mapenzi ya dhati na mumewe, lakini baadaye mambo yakabadilika, akaachwa, akalia na kuhuzunika.
Vivyo hivyo, anasema ilijirudia katika ndoa ya pili, mwanaume alimwonesha mapenzi ya dhati, naye akampenda mpaka wakafunga ndoa, lakini baadaye mume akabadilika na akamwacha tena, Zainab akaishia kuhuzunika na kulia kila wakati.
“Aliolewa ndoa ya kwanza akaachika, ikaja ya pili na sasa ya tatu. Akaona hana sababu ya kulia, ndiyo maana akaona asherehekee ili kuwatia moyo wengine waliopitia magumu kama yake,” anasema.
Katika ndoa hiyo ya tatu, anasema Zainab aliishi na mwenza wake kwa miaka mitatu na walipata watoto wawili pacha, lakini mambo hayakuwa sawa hadi wakaachana na mwenzake.
Anasisitiza uamuzi wa Zainab kufanya sherehe ya talaka umelenga kuwaonyesha wanawake wengine kwamba kuachana na changamoto za ndoa zisiwavunje moyo wakajifungia ndani kulia, bali wanapaswa kuwa imara.
Kuna ujumbe nyuma ya sherehe
Mtaalamu wa sosholojia, Dk Amina Mussa, anasema kwa baadhi ya watu, talaka huja baada ya miaka ya maumivu yasiyoonekana hadharani.
“Kwa mwanamke aliyekuwa katika ndoa yenye ukatili au dhuluma za kisaikolojia, talaka inaweza kuwa mwanzo wa uhai mpya. Sherehe ni kama anasema ‘nimejiokoa’,” anasema.
Anakwenda mbali zaidi na kueleza kuwa tukio hilo linafundisha umuhimu wa kujithamini, hasa kwa wanawake ambao kwa muda mrefu wamefundishwa kuvumilia hata pale uvumilivu unapohatarisha afya na uhai.
“Jamii imewazoesha wanawake kuficha maumivu yao. Tukio hili linaweza kuwaambia wengine kwamba kuondoka kwenye ndoa yenye madhara si kushindwa, bali ni uamuzi wa kujilinda,” anasema.
Ni hatari kwa taasisi ya ndoa
Kwa upande mwingine, Dk Amina anasema kusherehekea talaka hadharani ni hatari, hasa kwa vijana wanaojifunza maana ya ndoa kupitia mifano wanayoiona.
“Talaka inaruhusiwa pale inapolazimu, lakini si jambo la kufurahisha. Kuisherehekea kunaweza kudhoofisha maadili na kuwafanya watu wakose subira ya kutatua migogoro,” anasema.
Mtaalamu huyo anasema hata watoto wanaotazama talaka ikisherehekewa kuna hatari ya kukua na tafsiri hasi kuhusu familia, ahadi na uwajibikaji katika mahusiano ya ndoa.
Hoja kama hiyo imetolewa pia na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Malezi Tiki Tanzania, Florentine Senya, anayesema kusherehekea talaka kunajenga hamasa kwa ambao hawajaingia kwenye ndoa waone taasisi hiyo haina maana.
“Pia, kama watu wanafanya sherehe za kutalikiana, wanapoteza thamani halisi ya familia, ambayo ni taasisi ya kwanza ya kujenga jamii,” anasema.
Hatari nyingine, anasema, hamasa ya watu kuoana itapungua, watu watazaa na kuishi kwa kutengana, hatimaye watoto watakosa malezi ya wazazi wawili na kuwa na maadili dhaifu.
Iwapo talaka itafanywa kuwa sherehe, Senya anasema utafika wakati ndoa haitakuwa kitu cha maana, hivyo vijana wataona ni bora kuishi bila wenza.
Mazingira hayo, anasema, yatafanya jamii ione tendo la ndoa kuwa tukio la kustarehe na si jambo maalumu kwa wanandoa ili kujenga familia.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Malezi Tiki Tanzania, Senya anataja sababu za sherehe za talaka, akisema zinachochewa na watu wengi kuingia kwenye ndoa bila kutayarishwa, hivyo wanakutana na mambo mageni.
Wanapokutana na uhalisia wa changamoto za ndoa, anasema wanaona tabu kuishi na kuamua kutoka, wanapofanikiwa wanaona kama wamejikwamua, ndipo husherehekea.
Sababu nyingine, anasema, vijana wengi wanaingia kwenye ndoa ikiwa walishatumikia ndoa zisizo rasmi kadhaa kwa kuishi pamoja na wenza vyuoni na maeneo mengine.
Kwa kuwa walikuwa kwenye maisha ya ndoa isiyo rasmi, anasema wanashindwa kuenenda taratibu sahihi za ndoa rasmi ambazo ni kuheshimiana, kushirikishana, kushauriana na kutegemeana.
Pia, anasema vijana wengi wanapenda uhuru binafsi na wengi wamelelewa kukosa uvumilivu wakidhani kila kitu kinapatikana kwa urahisi.
“Hawana subira. Ndoa inawapa ugumu, kwa sababu ikitokea changamoto kidogo wanaona mzigo mzito na wanashindwa kuvumiliana,” anasema Senya.
Rehema Shabani, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema katika baadhi ya maeneo shughuli za aina hiyo zinafanyika na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, hasa wale walio karibu na mwenye shughuli.
Anasema pamoja na sababu nyingine, baadhi ya wanawake hufanya sherehe baada ya talaka kwa lengo la kutaka kurudishiwa fedha na zawadi walizotoa katika shughuli za wenzao, maarufu kama ‘kurudisha mtunzo’.
“Hivyo, mtu hutafuta jambo tu ilimradi afanye shughuli arudishiwe mtunzo wake aliotoa kwa wenzake. Katika baadhi ya shughuli hata kula keki ni lazima utoe pesa,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo, anasema suala la mtu kusherehekea talaka hadharani haliko sawa kimaadili.
Ingawa dini ya Kiislamu inaruhusu talaka pale inapobidi, anasema si jambo la kusherehekea, bila kujali umepitia madhila gani kwenye ndoa.
“Unakuta mtu anaishi katika ndoa ambayo haina amani, upendo wala furaha na anapitia madhila mengi. Sasa tutamlazimisha akae katika mazingira hayo moja kwa moja? Ndiyo maana taratibu za Kiislamu zikaweka utaratibu wa talaka,” anasema.
Anasema muhusika anaweza kuwa amefanya hivyo akiamini ameondokana na madhila aliyokuwa anayapitia, lakini kimaadili siyo sawa kufanya sherehe kufurahia talaka.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro anaeleza hiyo ni ishara kwamba watu wana changamoto katika akili, hivyo wanafanya sherehe kama njia ya kujipa matumaini na faraja kutoka kwenye maumivu na uchungu wa kupoteza.
Hata hivyo, anasema sherehe za talaka katika jamii ni tukio baya kwa sababu ndoa ni taasisi inayopaswa kutunzwa lakini wanapofanya sherehe kwa kuvunjika kwake, inaharibu heshima yake.
“Wanapofanya sherehe katika kuvunjika kwa ndoa wanatengeneza mazingira ya kuwafundisha maadili mabovu watoto na vijana. Thamani, umuhimu wa mahusiano na ndoa vinapungua, sio jambo la kushabikiwa linapaswa kukemewa,” anasema.
Anaeleza hilo linaitengenezea jamii mtazamo wa kuingia kwenye ndoa ikiwa imejiandaa kuivunja kwa kuwa inatambua talaka ni tukio la kufurahia.
Kwa mtazamo wa kisaikolojia, wakati mwingine shangwe na sherehe huwa pazia la kuficha maumivu, lakini si dawa ya majeraha ya kihisia, kama inavyoelezwa na mwanasaikolojia Dk Peter Luhanga.
“Mtu anaweza kucheka na kusherehekea leo, lakini maumivu yakajitokeza baadaye kwa msongo wa mawazo au hasira zisizotatuliwa. Talaka inahitaji msaada wa kisaikolojia, si sherehe pekee,” anasema.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, anasema hata kwake tukio hilo limekuwa jambo geni.
Anasema hilo linatokana na ukweli kwamba, kwa kawaida, ndoa ni jambo la heri na furaha, na talaka ni huzuni kwa kuwa si mpango wa wanandoa na viapo vyao.
“Kikawaida ndoa ni jambo la heri na furaha, na talaka ni jambo la huzuni, ambalo haitarajiwi lishangiliwe kwani haikuwa kwenye mpango wa wanandoa na viapo vyao. Ndiyo maana, kwa uzito wa taasisi ya ndoa, kuna sheria mahsusi,” anasema.
Anasema hata kama mtu binafsi au watu wachache waliona ni sahihi kuandaa sherehe, bado kushangilia anguko la ndoa kunaweza kuchochea matokeo hasi kwa wahusika na jamii kwa upana wake.
“Tukumbuke jamii ina makundi mengi mbalimbali yanayostawi kutegemeana na jinsi gani tunayafundisha na kuyarithisha mitazamo na matendo yetu, hasa watoto,” anaongeza.
Katika hali hiyo, Dk Gwajima anasema anaona haja ya kufanyika uchambuzi makini wa wataalamu wa ustawi wa jamii, saikolojia, imani, sheria ya ndoa na watu wazima wenye hekima.
Uchambuzi huo, anafafanua, utajikita kujua ilikuwaje sherehe hizo zinatokea, kwa ukubwa gani nchini, malengo ni nini, na matokeo chanya na hasi ni yapi na kwa nani.
“Watafanyia kazi na kuja na tamko la kitaalamu la elimu kwa umma kwani, vinginevyo, sherehe hizi zinaweza kuzoeleka na wengine wakaiga, kumbe nyuma yake kuna matokeo hasi kwenye maendeleo na ustawi wa jamii na makundi yake mbalimbali,” anasema Dk Gwajima.
