Sillah avunja mkataba, Yanga, Simba zishindwe zenyewe

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Azam raia wa Gambia, Gibril Sillah amevunja mkataba wake na ES Setif ya Algeria, baada ya nyota huyo kuichezea timu hiyo miezi sita tu, tangu alipoachana na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Julai 22, 2025.

Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho na kusaini mkataba hadi Juni 30, 2027, ingawa makubaliano ya kuusitisha yamefikiwa, huku ikidaiwa sababu kuu zilizochangia ni kutolipwa mshahara kwa miezi minne na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Taarifa zinaeleza mchezaji huyo ambaye awali alihusishwa naYanga baada ya kuondoka Azam, inadaiwa anaidai ES Setif mshahara wa miezi minne, jambo lililochangia kukaa chini na uongozi na kuamua kusitisha mkataba.

Vyanzo kutoka Algeria vinadai kiungo huyo maisha yake Afrika Kaskazini hayakuwa mazuri tofauti na matarajio ya wengi, jambo lililosababisha kuomba kusitisha mkataba wake.

Raia huyo wa Gambia alijiunga na Azam Julai 2, 2023 akitokea Raja Casablanca ya Morocco na kuitumikia kwa misimu miwili, akicheza mechi 68 za mashindano yote, akihusika na mabao 31 baada ya kufunga 21 na kuasisti 10.

Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 7, 1998, mbali na kuzichezea Raja Casablanca na Azam timu nyingine ni Samger FC na Fortune FC za Gambia, Teungueth FC (Senegal) na Jeunesse Sportive Soualem ya Ligi Kuu Morocco.

Kiungo huyo aliyehusika na mabao 13 ya Ligi Kuu 2024-2025 akiwa na Azam baada ya kufunga mabao 11 na kuasisti mawili, kwa 2025-2026 ameasisti mabao matano katika mechi 13 za mashindano yote alizoichezea ES Setif.