Simbachawene: Polisi lazima walinde raia kwa haki, usawa na uadilifu – Video

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewataka maafisa wakaguzi na askari wa Jeshi la Polisi wa vyeo mbalimbali kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa, weledi na uadilifu, akisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo ya msingi katika ulinzi wa raia na mali zao pamoja na ustawi wa taifa.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Askari uliofanyika katika Chuo cha Polisi Zanzibar tarehe 5 Januari 2026, Waziri Simbachawene ametoa maelekezo kwa maafisa wakaguzi na askari kutoka mikoa mitatu ya Unguja, akiwahimiza kuheshimu utawala wa sheria na kuwa na uwajibikaji wa hali ya juu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuwahudumia wananchi.

Amesema Jeshi la Polisi lina jukumu kubwa la kulinda raia na mali zao, na kwamba utekelezaji wa jukumu hilo unapaswa kuongozwa na misingi ya haki, usawa, uwajibikaji na uadilifu ili kulipeleka taifa mbele kimaendeleo.

Katika hotuba yake, Waziri Simbachawene amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutenga rasilimali nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu na vitendea kazi vya Jeshi la Polisi nchini.

“Baada ya kutambua mchango wenu mkubwa kwa usalama wa nchi yetu na kama lilivyo jukumu lenu kubwa la jeshi la polisi kwamba ni ulinzi wa raia na mali zao ili kuhakikisha ustawi, usawa, haki, uwajibikaji vinakuwa vitu vya msingi katika kulipeleka taifa letu mbele kimaendeleo”, ameeleza.

Aidha, Waziri Simbachawene amesema serikali inaendelea kulijenga na kuliboresha Jeshi la Polisi ili liendane na mahitaji ya sasa ya kiusalama pamoja na kuboresha maisha ya askari, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kulinda raia na mali zao. Amebainisha kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya polisi kuwa ya kisasa, yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama.

Sambamba na hilo, Simbachawene amesema serikali imejipanga kuongeza ajira ndani ya Jeshi la Polisi kwa kuajiri wataalamu wenye fani na utaalamu mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga Jeshi la Polisi lenye ushirikiano wa karibu na jamii.

Ameeleza kuwa polisi jamii ni njia rahisi na endelevu ya kuzuia na kupunguza vitendo vya uhalifu kupitia elimu, ushirikishwaji wa wananchi na kujenga imani kati ya polisi na jamii.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amewashukuru viongozi na askari wote wa Jeshi la Polisi Zanzibar kwa juhudi zao katika kulinda usalama wa raia na mali zao, akisisitiza kuwa taifa linahitaji Jeshi la Polisi la kisasa, lenye uadilifu na linalotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia haki na misingi ya kisheria.