TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’ leo Jumatano inatarajiwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA), Dar es Salaam ikirejea nyumbani baada ya kuweka historia katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars ilivuka hatua ya makundi kama moja ya timu nne bora zilizoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili baada ya kutoa sare dhidi ya Uganda na Tunisia kabla ya kuondolewa na wenyeji Morocco kwa kufungwa bao 1-0 katika hatua ya 16 bora.
Kutokana na mafanikio hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa ndege maalumu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner kwa ajili ya kuwachukua wachezaji wa Taifa Stars, benchi la ufundi pamoja na viongozi wao waliokuwa nchini Morocco na kuwarejesha nyumbani.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema uamuzi wa Rais Samia umetokana na kutambua heshima kubwa waliyoiletea Taifa Stars katika mashindano hayo makubwa ya Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba, ndege hiyo iliondoka Dar es Salaam jana, Jumanne saa 9:00 alasiri kuelekea Rabat, Morocco na ilitarajiwa kuwasili huko saa 4:30 usiku.
Ndege hiyo inaondoka Rabat leo, Januari 7 2026 na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa 2:00 usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JNIA).
Mbali na safari ya kurejea nyumbani, Rais Samia pia ameandaa hafla maalumu ya chakula cha mchana itakayofanyika Januari 10, 2026 katika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam kwa lengo la kuwapongeza Stars na wanamichezo wengine waliolitangaza vyema Taifa.
