Dar es Salaam. Huku Serikali ikiwa mbioni kuzindua Jukwaa la Vijana la Taifa, vijana kutoka makundi na vyama mbalimbali vya siasa wamejitokeza kupaza sauti zao, wakitaka wizara yenye dhamana kushughulikia kwa dhati vikwazo vinavyowakabili katika kushiriki na kunufaika na fursa za kisiasa. Wito huo unakuja wakati ambapo kundi la vijana, linalounda zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, bado linaonekana kutengwa au kunyimwa nafasi stahiki katika mifumo ya maamuzi ya kisiasa na kiutawala.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya ziara za mikoani alizofanya kukutana na makundi ya vijana, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Serikali imebaini changamoto nyingi zinazowakabili vijana na imeamua kuzishughulikia kwa kutumia jukwaa maalumu litakalowaunganisha kwa urahisi. Amesema jukwaa hilo litatumika kama njia ya kupokea maoni, kusikiliza malalamiko na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za maendeleo.
Nanauka amebainisha kuwa katika ziara hizo, changamoto kubwa zilizobainika ni pamoja na uhaba wa ajira, uhitaji wa mafunzo ya vitendo, upungufu wa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo, changamoto za mitaji kwa vijana wajasiriamali pamoja na ukosefu wa ushauri wa kibiashara. Amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kutumia teknolojia kama nyenzo kuu ya kurahisisha mawasiliano na kuwafikia vijana kwa wakati.
Kwa mujibu wa waziri huyo, uzinduzi wa Jukwaa la Vijana la Taifa unatarajiwa kufanyika Januari 10, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Jukwaa hilo linatajwa kuwa suluhisho muhimu kwa changamoto nyingi zinazowakabili vijana, hususan katika kuhakikisha sauti zao zinasikika na kupatiwa majibu ya vitendo badala ya kubaki katika malalamiko yasiyo na mrejesho.
Hata hivyo, vijana wamesisitiza kuwa mafanikio ya jukwaa hilo yatategemea zaidi uwezo wake wa kushughulikia changamoto za kisiasa wanazokumbana nazo. Wanasema kwa muda mrefu wamekuwa wakinyimwa nafasi za kushiriki kikamilifu katika siasa, hali inayowafanya kubaki kama wapambe wa wanasiasa wachache waliopo madarakani badala ya kuwa washiriki hai katika uongozi na maamuzi ya kitaifa.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVI-CUF), Abeid Rutozi, amesema licha ya vyama vingi vya siasa kuwa na jumuiya za vijana, bado kuna vikwazo vya kimfumo vinavyowanyima vijana fursa za kujieleza na kuendeleza ndoto zao za kisiasa. Ameeleza kuwa mazingira ya siasa nchini bado hayatoi ushindani wa haki kwa vijana wa vyama vyote.
Rutozi ameongeza kuwa ili vijana waweze kushiriki kikamilifu katika siasa, wizara inayohusika inapaswa kushughulikia hofu iliyojengeka miongoni mwa vijana kuhusu usalama na uhuru wao wa kisiasa. Amesema kuna imani iliyoenea kwamba kijana asiyeonesha ukaribu au utii kwa Chama Cha Mapinduzi au Serikali anaweza kujikuta katika mazingira hatarishi, hali inayozima ujasiri wa vijana wengi kushiriki siasa kwa uwazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, amesema vijana ndio waathirika wakubwa wa tatizo la ajira, changamoto za kiusalama na ukosefu wa uwakilishi wa kutosha katika vyombo vya maamuzi. Ameeleza kuwa mfumo wa Katiba ya mwaka 1977 umeweka mazingira ya chaguzi zisizo huru, hali inayowakatisha tamaa vijana wengi kugombea nafasi za uongozi.
Nondo amesema vijana wanaokataa kukata tamaa na kuamua kugombea nafasi za uongozi hukumbana na changamoto nyingi ikiwemo vitisho, vurugu, matumizi ya nguvu kupita kiasi na dosari katika taratibu za uchaguzi. Ameitaka mifumo ya uchaguzi kuwa huru na vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, kujitenga na siasa ili kujenga imani kwa vijana.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa NCCR Mageuzi, Nicholaus Jovin, amesema mifumo ya ndani ya vyama vya siasa inawabana vijana wengi na kuwanyima fursa za uwakilishi. Ameeleza kuwa mara nyingi nafasi za uongozi hutolewa kwa vijana wenye ushawishi au wanaoungwa mkono na viongozi wakubwa, huku vijana wenye uwezo lakini wasio na “mtandao” wakibaki pembeni.
Jovin amesisitiza kuwa mabadiliko ya Katiba ni muhimu, ikiwemo kuruhusu uwepo wa mgombea binafsi, hatua itakayowapa vijana wengi waliokwama ndani ya vyama nafasi ya kugombea na kushiriki siasa bila vikwazo vya mifumo ya vyama.
Kwa upande wa vyama vya siasa, mitazamo imekuwa tofauti. Baadhi ya viongozi wamekiri kuwa vijana ni chachu ya mabadiliko kutokana na ubunifu wao na matumizi ya teknolojia. Msemaji wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), John Mrema, amesema vijana wana wajibu mkubwa wa kujenga vyama imara vya siasa ambavyo vitasimamia maslahi yao ya sasa na ya baadaye.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), Rashidi Rai, amesema vijana wengi hukosa ajenda ya pamoja, hali inayowafanya kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa maslahi binafsi badala ya kusimamia masuala muhimu kama elimu, ajira, afya na usawa wa kijinsia.
Kihistoria, wito wa kuwa na Jukwaa la Vijana la Taifa si jambo jipya. Tangu miaka ya 1980, kumekuwepo juhudi mbalimbali za kuanzisha chombo cha kitaifa cha sauti za vijana, lakini juhudi hizo hazikufikia mafanikio. Mwaka 2015, Bunge lilitungwa sheria ya Baraza la Vijana, huku kanuni zake zikitangazwa mwaka 2017, lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu hadi sasa.
Sheria hiyo inalenga kuwaunganisha vijana wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini au kikabila, na kuweka muundo wa baraza kuanzia ngazi ya kata hadi taifa.
Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana la Taifa unaotarajiwa Januari 10, 2026 unatajwa kuwa fursa mpya ya kufufua dhamira hiyo na kuwapa vijana jukwaa la kweli la kusikilizwa na kushirikishwa katika maendeleo ya taifa.
