Wachina wa mabilioni wapandishwa kizimbani kwa utakatishaji fedha

Dar es Salaam. Raia wawili wa China waliokamatwa na rundo la fedha ndani ya nyumba wanamoishi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha zaidi ya Sh2 bilioni.

Wachina hao, Weisi Wang (44) mkazi wa Masaki, jijini Dar es Salaam na Dong, China, na mwenzake na Yao Licong (32), mkazi wa Masaki, jijini Dar es Salaam na Jiangxi nchini China.

Akiwasomea mashtaka leo Jumatano, Januari 7, 2026, Wakili wa Serikali, Benjamini Muroto, amesema washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili, moja la kuongoza genge la uhalifu na la pili la kutakatisha fedha.

Katika shtaka la kwanza, Wakili Muroto amedai kwa nyakati tofauti kati ya Desemba Mosi, 2024, na Desemba 30, 2025, washtakiwa hao katika maeneo tofauti katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Unguja, Zanzibar na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliratibu uhalifu wa kughushi, kuiba taarifa za kadi za kutolea fedha kwenye mashine za ATM, kukwepa kodi na kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Raia wa China, Weisi Wang (41) na Yao Licong (32) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Januari 6, 2026. Picha na Hadija Jumanne

Amedai walitenda kosa hilo kinyume na Aya 4(1)(a) ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2), vyote vya Sheria ya Uhalifu wa Kupanga na Uhujumu Uchumi, Sura ya 200, Rekebu ya 2023.

Katika shtaka la pili, Wakili Muroto amedai katika tarehe hizo na maeneo hayo, washtakiwa hao walitenda kosa la utakatishaji fedha Dola 707,875 za Marekani (zaidi ya Sh1.7 bilioni) na Sh281.71 milioni, huku wakijua fedha hizo ni matokeo ya kosa la uhalifu tangulizi, yaani kuongoza genge la uhalifu.

Amedai walitenda kosa hilo kinyume na vifungu vya 12(1)(a) na 13(1)(a) vya Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423, Rekebu ya mwaka 2023.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, amewaeleza washtakiwa hao kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi, hivyo hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza, na kwamba shtaka la utakatishaji fedha linalowakabili halina dhamana.

“Hii si mahakama ya uhujumu uchumi, hivyo hamtatakiwa kujibu chochote. Uchunguzi utakapokamilika mtapelekwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, ambapo mtapewa haki ya kusikilizwa,” amesema Hakimu Nyaki na kuongeza:

“Pia kwa kuwa mnakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha, shtaka hili halina dhamana, hivyo mtakaa mahabusu mpaka kesi hii itakapohamishiwa Mahakama Kuu.”

Wakili Muroto ameieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Nyaki ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2026, itakapotajwa kuangalia mwenendo wa upelelezi.

Taarifa za kukamatwa kwa Wachina hao na mabunda ya pesa yaliyokuwa ndani ya mifuko mikubwa ya sandarusi zilitolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, aliyesema watuhumiwa walikamatwa kwa msaada wa taarifa kutoka kwa raia wema na kwamba waliwakamata na jumla ya Sh6 bilioni.

Kipande cha video kilichosambaa mitandaoni kilionesha fedha hizo zikiwa kwenye mifuko maarufu (shangazi kaja).

Hata hivyo, kabla ya Wachina hao kupandishwa mahakamani, Takukuru Mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam ilizungumza na waandishi wa habari na kuelezea operesheni maalumu iliyofanikisha kukamatwa kwao.

Watuhumiwa hao wanahusishwa na matukio mbalimbali ikiwemo utakatishaji fedha, wizi wa taarifa za kadi za benki na uhujumu uchumi.

Mkuu wa Takukuru wa mkoa huo, Christian Nyakizee, amesema katika operesheni maalumu iliyofanyika Januari 5, 2026, walifanikiwa kuwakamata raia hao wakiwa na fedha taslimu Dola 707,075 za Marekani, sawa na Sh1.732 bilioni na Sh281.45 milioni, zikiwa ndani ya gari katika mifuko ya sandarusi.

“Fedha hizo zinashukiwa kuwa matokeo ya fedha zilizotakatishwa kupitia taarifa za kadi za benki zilizotwaliwa kutoka kwa watu mbalimbali nje ya nchi,” amesema Nyakizee.

Ukamataji huo umetokana na matokeo ya operesheni maalumu ya miezi saba tangu Mei 2025, iliyoendeshwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), benki za biashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, amesema watuhumiwa hao wameshindwa kuthibitisha uhalali wa upatikanaji wa fedha hizo kwani hawana kampuni au biashara halali zinazoeleza chanzo cha fedha walizokutwa nazo, wala hawana uthibitisho au stakabadhi za jinsi walivyopata fedha za kigeni walizokutwa nazo.

Nyakizee amesema mtuhumiwa Licong alikuwa akitafutwa na taasisi hiyo kwa tuhuma za ufunguaji wa kampuni hewa tano zinazochunguzwa kwa makosa ya ukwepaji kodi na utakatishaji fedha kiasi cha Sh1.8 trilioni, ambazo zinadaiwa hazijatozwa kodi tangu mwaka 2019.

Akielezea kuhusu taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kukamatwa na Sh6 bilioni, Nyakizee amesema ukamataji ulifanyika kwa kushuhudiwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, ambaye alithibitisha watuhumiwa walikamatwa na kiasi kilichotajwa.

“Ieleweke maofisa wa Takukuru ndiyo waliomuita Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ili ashuhudie tukio hili kwa mujibu wa sheria na taratibu za ushahidi na upekuzi,” amesema Nyakizee.

Mbali na hilo, Nyakizee amesema wamewakamata watuhumiwa wengine zaidi ya 137 ambao wamepekuliwa na kuhojiwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam pamoja na Visiwa vya Zanzibar.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini zaidi ya Sh18 bilioni zimetakatishwa kwa kutumia malipo ya mashine za POS, payment links, majukwaa ya e-commerce pamoja na kumbukumbu namba kwa ajili ya huduma za utalii, afya, malazi, usafiri wa anga na kodi za ndani.

Amesema watuhumiwa wakuu wa wizi wa taarifa za kadi wanatoka katika nchi za Cameroon, Nigeria, Pakistan, Bulgaria, Macedonia, Poland, Romania na China, huku wakishirikiana na baadhi ya Watanzania waliotumika kupitisha fedha hizo kupitia akaunti zao binafsi na za kampuni.

“Ni genge la kihalifu la kimataifa linalojihusisha na utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na uhujumu uchumi. Fedha zilipitia kwenye kadi kisha kuingizwa kwenye akaunti za kampuni binafsi, nyingi zikiwa za vijana Watanzania waliopata huduma za kibenki katika benki mbalimbali hapa nchini,” amesema.

Amesema baada ya fedha kuingia kwenye akaunti za kampuni, zilikuwa zinatolewa taslimu na kugawanywa kwa makubaliano ya asilimia fulani kati ya wahusika.

Katika hatua ya kisheria, amesema mashauri matatu tayari yamefunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kwa makosa ya wizi wa mtandao, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi. Mashauri hayo ni ECC 21633/2025, ECC 29134/2025 na ECC 29143/2025.

“Kati ya washtakiwa waliopo mahakamani ni raia wa China saba, raia mmoja wa Bulgaria na Mtanzania mmoja. Hatua nyingine za kisheria zinaendelea kwa watuhumiwa wengine pamoja na jitihada za kurejesha fedha zilizoibiwa,” amesema.

Pia amesema zaidi ya Sh1 bilioni zimerejeshwa kwa waathirika, huku Sh3 bilioni zikizuiwa kwenye akaunti za watuhumiwa kusubiri kukamilika kwa uchunguzi.