Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Januari 20, 2026 kumsomea hoja za awali (PH) Khalid Kitambi maarufu Dee na mwenzake Anitha Kibona, wanaokabiliwa na kesi ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni usafirishaji haramu wa biandamu na kufanya kazi ya uwakala wa ajira bila kuwa na kibali kutoka kwa kamishna wa kazi.
Tarehe hiyo imepangwa leo Jumatano, Januari 7, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Awali, wakili wa Serikali Tumaini Mafuru alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa PH, lakini upande wa utetezi walikuwa bado hawajapata nyaraka za kesi hiyo kutoka kwenye mtandao wa Mahakama.
“Nyaraka zote tumeshasajili kwenye mfumo, lakini upande wa utetezi tunaona bado hawajazipata, hivyo kutokana na hali hii tunaomba mahakama itupangie tarehe fupi ili waweze kuzipata na tuje kuwasomea hoja za awali,” amedai Mafuru.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, hakimu Lyamuya alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 20, 2026.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa katika tarehe zisizofahamika Agosti 2024, eneo la Sinza Mori, walimpa mafunzo ya kingono Natasha Mohamed na kumuahidi watamsafirisha kwenda nje ya nchi kufanya kazi huku wakiwa na nia ya kumnyanyasa kingono.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa Septemba 17, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walimsafirisha Natasha kutoka Dar es Salaam kwenda Guangzhou, China kufanya kazi, huku wakiwa na nia ya kwenda kumnyanyasa kingono.
Shtaka la tatu, washtakiwa kwa pamoja tarehe zisizofahamika kati ya Agosti na Septemba 2024 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, walijihusisha na kufanya kazi ya Uwakala wa Ajira kwa Natasha bila kuwa na kibali kutoka kwa kamishna wa kazi.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 26, 2025.
