Moshi. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, ameelekeza vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi nchini (Veta) kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza ujuzi wa teknolojia mpya unaoendana na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha vyuo vya Veta vinaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira nchini.
Naibu Waziri Wanu amesema hayo leo, Januari 7, 2026, wakati alipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kilimanjaro (Veta Moshi), akisisitiza kuwa ni muhimu kuimarisha mafunzo yanayofaa ili vijana watakaohitimu wawe wamoja na teknolojia za kisasa na mahitaji halisi ya ajira.
“Ni muhimu Veta ihakikishe kuwa, ushirikiano huu unaimarishwa ili kuongeza ubora wa mafunzo, maelekezo yangu kwa uongozi wa Veta ni kuongeza wigo wa ushirikiano na makampuni mengi zaidi,” amesema Wanu.
Aidha, amesisitiza utekelezaji wa mpango huo utafanyika kwa kuzingatia muelekeo wa Taifa uliowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, pamoja na sera za sekta husika na miongozo mbalimbali ya kitaifa, ili kuhakikisha mikakati ya mafunzo ya Veta inalingana na malengo ya maendeleo ya nchi.
“Ninasisitiza kuwa ushirikiano baina ya Veta na sekta binafsi ujumuishe ukuzaji ujuzi katika teknolojia mpya na za kisasa zinazoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda.
“Nimefarijika sana kujionea karakana za mafunzo zilizosheheni vifaa vya kisasa na vya thamani kubwa, hii inathibitisha kuwa chuo hiki ni cha kimkamati kinachochangia kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi katika sekta za madini, uzalishaji viwandani na teknolojia ya kusafirisha mafuta na gesi kwa mfano katika mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP),” amesema Naibu Waziri huyo
Mkuu wa chuo hicho, Lupakisyo Mapamba amesema chuo hicho kinaendelea kushirikiana na taasisi pamoja na makampuni mbalimbali katika kutoa mafunzo.
Aidha, amesema chuo hicho kinatoa bunifu mbalimbali kama majiko ya kutumia nishati safi na sufuria za kupikia jiko, na kwamba mafunzo wanayoyatoa yanatambulika Kitaifa.
Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Ibrahim Shayo amesema kutokana na ubunifu unaofanywa na chuo hicho atatoa ufadhili kwa vijana 10 kila mwaka ili kupata juzi mbalimbali katika chuo hicho zitakazowasaidia kujiajiri.
