Yanga Princess yaiadhibu Mashujaa Queens WPL

LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) imeendelea leo zikipigwa mechi tano ikiwemo ya Yanga Princess dhidi ya Mashujaa ambapo Wananchi hao waliondoka na ushindi wa mabao 4-1 Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Asha Djafari dakika ya tisa. Asha amesajiliwa kikosini hapo hivi karibuni na mechi ya leo ilikuwa ya pili kwake, huku mabao mengine matatu yakifungwa na Jeaninne Mukandayisenga dakika ya 40, 60 na 82, ikiwa ni hat trick huku lile moja la Mashujaa likiwekwa kambani dakika ya 77 na Vaileth Machela.

Pointi tatu ilizopata Yanga imeifanya ifikishe pointi 18 sawa na Simba iliyopo kileleni na sasa inapanda hadi nafasi ya pili na kuishusha JKT iliyokuwa na pointi 16.

Katika mechi hiyo Mukandayisenga alionekana kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Mashujaa  walioshindwa kumzuia kutia mpira nyavuni kutokana na kasi yake na nguvu.

Hat-trick ya leo inamfanya Mukandayisenga kufikisha idadi ya mabao saba sawa na Winifrida Gerald wa JKT Queens.

Mechi nyingine za raundi ya saba zilizopigwa jioni ya leo, Alliance ikiwa nyumbani Uwanja wa Nyamagana imeitandika Geita Queens kw mabao 2-1, Bilo imepoteza 2-1 mbele ya Bunda Queens, Tausi ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Ruangwa Queens na Ceasiaa Queens ikitandikwa 2-1 na Fountain Gate.

Ligi hiyo itaendelea kesho Alhamisi kwa mechi moja ya wababe wa WPL kati ya watetezi JKT Queens dhidi ya Simba Queens, mechi hiyo itapigwa saa 12 kamili jioni Uwanja wa Azam Complex.