Dar es Salaam. Huduma ya Afya ya Aga Khan Tanzania (AKHS, T) imepiga hatua katika safari yake ya mageuzi ya kidijitali baada ya uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa kumbukumbu za wagonjwa (EHR) katika mtandao wake wa kitaifa wa huduma za afya.
Mfumo huo wa Meditech unatarajiwa kurahisisha kazi kwa wataalamu na kuhakikisha wagonjwa wanaohama kutoka kituo kimoja kwenda kingine wanapata huduma endelevu bila kurudia vipimo au taratibu za karatasi.
Utekelezaji huo, umezingatia Mpango wa One Health wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN).
Hospitali ya Rufaa ya Aga Khan, Dar es Salaam na ya kufundishia yenye vitanda 170, ilianza rasmi kutumia mfumo huo mwaka 2025, huku mipango ikiwa ni kuutekeleza katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Karachi, mwaka 2026.
Hatua hiyo ni katika kuboresha utoaji wa huduma endelevu za afya Tanzania nzima.
AKHS, T inaendesha mfumo jumuishi wa huduma za afya katika hospitali ya Dar es Salaam inayoungwa mkono na Kituo cha Tiba cha Aga Khan Mwanza pamoja na vituo 20 vya Afya vya Outreach vilivyosambaa nchi nzima, vinavyotoa huduma maalumu moja kwa moja kwa jamii.
“Kwa pamoja, mfumo huu jumuishi wa huduma za afya unahudumia zaidi ya wagonjwa milioni moja kila mwaka.
Vituo hivi vyote sasa vimeunganishwa kikamilifu kupitia jukwaa la Meditech, inayowezesha uhamishaji salama na wa haraka wa kumbukumbu za wagonjwa, taarifa za kitabibu na za kifedha,” amesema ofisa mwendeshaji mkuu wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan nchini, Sisawo Konteh.
Amesema hiyo itawawezesha watoa huduma za afya kupata taarifa za kitabibu kwa wakati halisi kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi, na kuhakikisha wagonjwa wanaohama kutoka kituo kimoja kwenda kingine wanapata huduma endelevu bila kurudia vipimo au taratibu za karatasi.
“Mfumo huu wa pamoja unaonyesha dhamira yetu ya kutoa huduma za afya za viwango vya juu zaidi, na unaakisi dhana ya One Health ya AKDN, inayounganisha afya ya binadamu, jamii na mazingira,” amesema Konteh.
Pia amesema mfumo huo utaweza kutumika katika Mtandao wa Kimataifa wa AKDN.
“Wagonjwa wa Tanzania wanaopata matibabu katika vituo vya AKDN vilivyopo nchi kama Kenya, Pakistan na kwingineko, watanufaika na huduma za haraka na salama zaidi, zinazotegemea historia yao ya kitabibu. Hatua hii itabadilisha kwa kiasi kikubwa huduma za utalii wa tiba na upatikanaji wa huduma bora za afya kimataifa,” amesema Konteh.
Konteh amesema mageuzi haya yanaendana na juhudi za Serikali ya Tanzania za kupanua upatikanaji wa huduma za afya bora na nafuu.
Amesema kwa kurahisisha usimamizi wa taarifa za kitabibu na kupunguza urudiaji wa huduma, mfumo huu unasaidia kupunguza gharama, kuongeza ufanisi na kuimarisha matokeo ya afya kitaifa.
Kupitia Patient Portal, wagonjwa sasa wanaweza kupata taarifa zao za afya kwa usalama, matokeo ya vipimo na kupanga miadi, hatua inayowaweka katikati ya huduma zao na kuhamasisha usimamizi makini wa afya binafsi.
Amesema pia mpango huu utapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya karatasi, na hivyo kuunga mkono juhudi za za kulinda mazingira na kujenga jamii yenye afya na usalama zaidi.
“Hii inaendana na Mpango wa AKDN wa Go Green na dhamira yake ya kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2030.
Taasisi hii tayari imehamia kwa kiwango kikubwa katika matumizi ya nishati ya jua, kubadilisha vifaa kwa teknolojia rafiki kwa mazingira, na kununua magari ya umeme ili kupunguza kiwango chake cha uchafuzi wa mazingira,” amesema Konteh.