Dar es Salaam. Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, Serikali inatarajia kutangaza ajira 1,000 za madereva na mafundi wa magari pamoja na viyoyozi nje ya nchi mwishoni mwa mwezi huu.
Ajira hizo ni sehemu ya jumla ya ajira 8,000 zinazochakatwa na Serikali, ambapo kati ya hizo, 1,000 zinahusisha fursa mbalimbali ikiwemo ajira 90 za madereva wa magari ya kawaida na mabasi, huku zilizobaki zikiwa ni za mafundi wa magari na viyoyozi. Ajira zote hizo zinatarajiwa kutolewa nchini Qatar.
Akizungumza leo Alhamisi, Januari 8,2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 109 wanaoelekea kufanya kazi nje ya nchi, ikiwemo Dubai, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Deus Sangu, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuongeza fursa za ajira, kuinua kipato cha vijana na kuchochea maendeleo ya Taifa.
“Kwanza tuwapongeze vijana 109 waliopata fursa hizi za ajira nje ya nchi. Mwishoni mwa mwezi huu, tutatangaza ajira nyingine 1,000 kati ya ajira 8,000 tunazozichakata, zikiwemo za madereva wa magari ya kawaida na mabasi pamoja na mafundi wa magari na viyoyozi,” amesema Sangu.
Amesema ajira hizo zitatangazwa kwa kufuata utaratibu uliopo kupitia mawakala wa ajira wa sekta binafsi wanaotambuliwa na Serikali, kwa kushirikiana na ofisi za ajira ngazi ya mikoa na wilaya, ili kuhakikisha hata vijana wa vijijini wanapata fursa hizo.
Amesema mchakato wa kuwapata vijana hao na ajira zingine zinazotarajiwa kutangazwa mchakato utaanza ngazi ya wilaya, mkoa na mchujo wa mwisho utakuwa unafanyika ngazi ya kanda zote.
“Tumeanza mwaka mpya kwa dhamira ya kujenga uchumi shindani unaotengeneza ajira, sambamba na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 inayoweka kipaumbele kwa ajira za vijana,” amesema.
Sangu amesema licha ya vijana kwenda kufanya kazi nje ya nchi, Serikali itaendelea kuwafuatilia kupitia balozi zake ili kuhakikisha wanapata haki zao na kulindwa dhidi ya manyanyaso, huku akiwahimiza kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu ili kujenga uaminifu.
“Mtakwenda kufanya kazi kwa mikataba ya heshima, na Serikali itakuwa bega kwa bega nanyi kuhakikisha mnalindwa. Tunawatambua kama watoto wetu na tutaendelea kuwafuatilia kwa karibu,” amesema.
Ameongeza kuwa vijana hao wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, kuitangaza vyema nchi yao na kuepuka tabia za uvivu au vurugu.
“Ajira za nje ya nchi si maumivu bali ni uwekezaji kwa maendeleo ya Taifa. Ni fursa ya kujifunza teknolojia na uzoefu ambao haupatikani kwa urahisi hapa nchini,” amesema.
Akitoa tathmini ya utekelezaji wa Serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miezi miwili tangu kuingia madarakani, Waziri Sangu amesema jumla ya ajira 1,432 zimepatikana, zikiwemo ajira 109 ambazo vijana wake wameagwa leo.
Waziri Sangu amesema, “Huu ni utaratibu ambao hata Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inasisitiza utoaji wa ajira kwa vijana. Serikali tumejizatiti kusaka ajira za umma na binafsi, ndani na nje ya nchi, na tumekuwa na mahusiano mazuri na nchi za nje.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Zuhura Yunus, amesema vijana 109 walioagwa wanaelekea kufanya kazi kupitia mfumo rasmi wa ajira, jambo linalothibitisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanapata ajira salama na zenye ulinzi wa kisheria.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi, kutangaza ajira kwa uwazi na kusimamia mikataba ili kulinda haki na masilahi ya vijana.
“Serikali imeamua kusimamia ajira za nje kwa mfumo rasmi badala ya kuziacha zifanyike kiholela. Ajira za nje ni salama endapo zitazingatia taratibu na mifumo ya Serikali,” amesema Yunus.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Muungano wa Mawakala Binafsi wa Ajira Tanzania Nje ya Nchi (TRA), Abdallah Mohamed, amesema jukumu la muungano huo ni kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha Watanzania wanapata ajira zenye staha.
