DAKIKA nane alizocheza beki Attohoula Yao zimetosha kumtoa chozi daktari wa viungo wa Yanga, Youssef Ammar aliyedai sababu ya chozi lake kuwa haikuwa rahisi kumrudisha uwanjani na anamuona akirudi kwa ubora mkubwa.
Yao ambaye amekaa nje kwa zaidi ya miezi saba, alipata nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya TRA United akiingia dakika ya 82 kuchukua nafasi ya Kibwana Shomari kwenye Kombe la Mapinduzi juzi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Youssef amesema amefurahishwa na dakika chache alizozipata Yao baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza jeraha la goti huku akimtabiria makubwa.
“Nimefurahi sana hayakuwa machozi ya huzuni, ni furaha iliyopitiliza. Yao amekaa nje ya uwanja muda mrefu. kitendo cha kupata nafasi ya kucheza mechi ya mashindano kwangu kimenipa amani, kwani nimepambana naye muda mrefu,” amesema.
“Yao atakuwa bora sana kama atapata nafasi ya kuendelea kuitumikia Yanga. Ni mchezaji mpambanaji, hakubali kushindwa na anapenda kazi yake. Akirudi na kupata muda wa kucheza atarejea akiwa bora sana.”
Amesema mchezaji huyo amekuwa akizingatia programu zote anazopewa kitabibu, hivyo yupo timamu kimwili na anachotakiwa kufanyiwa sasa ni kupewa dakika chache kama alivyopata juzi ili aweze kurudi mdogomdogo.
“Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anajituma, akirudi kwenye utimamu wake namuona akikimbiza sana eneo analocheza na alikuwa ananiahidi kuwa kwa kazi niliyomfanyia atakuja kunionyesha kitu bora kama zawadi.
“Ukiondoa mazungumzo yake mimi kama kocha katika muda niliokaa naye nimegundua ni mchezaji ambaye anaipenda kazi yake, lakini pia ana nidhamu sana ya mpira. Nimefurahishwa na kurudi kwake uwanjani.”
Kocha Pedro Goncalves amesema: “Tumemuona Yao amerudi. Ni jambo zuri. Nimefurahi kwa sababu inazidi kuimarisha kikosi hasa eneo la ulinzi. Ni mchezaji ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na sasa yupo fiti.”
