Basi lakutwa na shehena ya skanka

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha havitumiki kusafirisha dawa za kulevya na kuwa haitasita kumchukulia hatua mmliki endapo chombo chake kitakutwa na dawa hizo haramu.

Onyo hilo limekuja kufuatia kuongezeka kwa matukio ya kukamatwa dawa za kulevya zinazosafirishwa kwa njia ya barabara, likiwemo la hivi karibuni ambapo kilo 20.03 za skanka zilikamatwa kwenye basi linalofanya safari zake kati ya Tanzania na Msumbiji.

Dawa hizo za kulevya zilifungashwa kwenye pakiti zilizofungwa kwenye balo la mitumba na kuwekwa kwenye eneo la mizigo ambalo halionekani kwa urahisi.

Ukaguzi uliofanywa na mamlaka hiyo ulibaini gari hilo kufanyiwa maboresho ya muundo ili kuwezesha mizigo kuingizwa bila kubainika, jambo ambalo ni kinyume linalokinzana na sheria zinazohusu usafirishaji nchini Tanzania.

Hata hivyo, imebainika gari hilo licha ya kumilikiwa na Mtanzania, usajili wake umefanyika nchini Msumbiji na limekuwa likibeba mizigo kati ya nchi hizo mbili.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimbo amesema hatua ya kubadilisha muundo wa gari hilo ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya, hivyo mamlaka hiyo inakwenda kuongeza ufuatiliaji katika vyombo vya moto.

“Haiwezekani gari linabadilishwa muundo halafu mmiliki useme haufahamu, tutakukamata na sheria itachukua mkondo wake kama ambavyo imefanyika kwa mmiliki wa gari hili, hatuwezi kukubali kurudishwa nyuma katika juhudi zetu za mapambano dhidi ya dawa za kulevya,” amesema Lyimo.

Akizungumzia hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri Ardhini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra), Halima Mtaji amesema gari hilo halijasajiliwa nchini kutokana na mmiliki kushindwa kukidhi vigezo vya kupata leseni.

“Huyu alikuja lakini kabla ya kupewa leseni kuna vigezo na inaonekana alishindwa kuvikamilisha hivyo hakurudi tena hadi tuliposikia limekamatwa likiwa na dawa haramu za kulevya. Tulichofanya ni kusitisha leseni ya magari yake yote.

Taarifa zetu zinaonyesha ana magari mawili yenye leseni na pia yapo mengine, hivyo tutayatafuta na hayo na kuyazuia yasiingie barabarani,” amesema Halima.

Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imemkamata raia wa Kenya Jefferson Kilonzo (35) aliyejulikana kama muuza chai ya maziwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin gramu 131.88.

Mtuhumiwa huyo amekamatwa alikokuwa akiishi Sinza jijini Dar es Salaam kufuatia taarifa za watu waliomtilia shaka kwamba huenda kuna anachokifanya zaidi ya biashara yake ya chai ya maziwa.

Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali Lyimo, mienendo ya maisha ya mtuhumiwa huyo iliwatia shaka watu waliokuwa jirani naye ndipo walipotoa taarifa na uchunguzi ukaanza kufanyika dhidi yake.

“Kuna namna inafikirisha, mtu atoke kwao aende nchi nyingine kuuza chai, pia maisha yake yalikuwa yanaonyesha ana chanzo kingine cha mapato zaidi ya hiyo biashara ya chai ya maziwa.

“Tulipopata taarifa tukaanza kumfuatilia na ndipo tukamkuta na kiasi hicho cha heroin nyumbani kwake.

“Baada ya kumhoji tulibaini aliishi nchini tangu mwaka 2023 na alitumia biashara ya kuuza chai ya maziwa kufisha biashara yake ya dawa za kulevya,”

Kufuatia hilo Lyimo ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoishi jirani na wageni ambao hawajulikani wanafanya nini.

“Inawezekana unaishi jirani na mgeni na mienendo haieleweki, usipoteze muda chukua hatua kwa kutoa taarifa kwa mamlala husika, kinyume na hapo tutaruhusu hawa wageni waingize dawa za kulevya na kuharibu vijana wetu,” amesema.