BoT: Uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 5.9  mwaka 2025

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza kuwa, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 pungufu kwa asilimia 0.1 ya lengo mwaka 2025 huku thamani ya shilingi ikiongezeka thamani kwa asilimia 0.8 katika robo ya nne ya mwaka 2025.

Akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) iliyofanya kikao chake jana Jumatano, Januari 07, 2026 Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema kiwango hicho cha ukuaji wa uchumi na kuimarika kwa shilingi kimetokana na ongezeko la shughuli za uchumi na kuimarika kwa mfumko wa bei ndani nje.

“Kamati ya Sera ya Fedha ilibaini kuwa uchumi wa Tanzania bara uliendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha ya takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ikilinganishwa na makadirio ya ukuaji wa asilimia 6.

“Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, madini na ujenzi. Kwa upande wa Zanzibar, ukuaji wa uchumi wa mwaka 2026 unakadiriwa kufikia asilimia 6.8, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani,” amesema Tutuba.

Kwa mwaka huu, Tutuba amesema ukuaji wa uchumi wa Tanzania mwaka 2026 unakadiriwa kufikia asilimia 6.8, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.

Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa wastani wa asilimia 20.3 kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, uchumi wa Tanzania bara unatarajiwa kukua kwa asilimia 6, na uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.

Kuhusu sekta ya nje Tutuba amesema uchumi wa dunia kwa mwaka 2025 uliendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha licha ya athari zinazotokana na ongezeko la ushuru wa bidhaa za forodha, migogoro ya kisiasa, pamoja na kutokutabirika kwa matarajio ya hali ya uchumi duniani. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linakadiria ukuaji wa uchumi wa dunia kufikia asilimia 3.2 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2024 na unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi hiyo mwaka 2026.

Katika robo ya nne ya mwaka 2025, bei ya mafuta ghafi ilipungua na kufikia kati ya Dola 62–65 za Marekani kwa pipa, na inatarajiwa kubaki katika viwango hivyo kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 kutokana na ongezeko la uzalishaji, sambamba na kupungua kwa mahitaji duniani.

Amesema hali hiyo inatarajiwa kuendelea kupunguza mfumuko wa bei na mahitaji ya fedha za kigeni hapa nchini, hivyo kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi, ikizingatiwa kwamba bidhaa za petroli huchangia takriban asilimia 17 ya gharama ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Amesema mfumuko wa bei umeendelea kupungua na kufikia karibu au chini ya malengo ya benki kuu katika nchi nyingi, kutokana na kupungua kwa bei za nishati na utekelezaji wa sera za fedha katika nchi husika zilizopunguza viwango vya ukwasi katika vipindi vilivyopita.

Kwa kuzingatia mwenendo huu, Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kuwa mwenendo wa uchumi wa dunia utaendelea kusaidia mfumuko wa bei nchini kubaki ndani ya lengo la mwaka 2026.

“Bei ya dhahabu iliongezeka na kufikia kiwango cha juu cha Dola 4,421.65 za Marekani kwa wakia, na inatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwaka 2026. Mwenendo wa bei ya dhahabu unatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuendelea kuimarisha thamani ya shilingi hapa nchini.”

Mfumko wa bei BoT imeeleza kuwa, umeendelea kuwa tulivu, ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 kama ilivyokuwa imepangwa.

Katika robo ya nne ya mwaka 2025, mfumuko wa bei kwa Tanzania bara ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.5.

Amesema mwenendo huo mzuri ulitokana na utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha na mazingira mazuri ya kiuchumi duniani yaliyopunguza ongezeko la mfumuko wa bei kutoka nje ya nchi.

Kamati inatarajia kuwa, mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 kwa robo hii.

Aidha Tutuba amesema, vihatarishi katika utoaji wa mikopo vimeendelea kupungua huku uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ulipungua na kufikia asilimia 3.1, chini ya ukomo unaovumilika wa asilimia 5 huku mifumo ya malipo imeendelea kuwa thabiti, ikifanya kazi kwa ufanisi katika maeneo ya mijini na vijijini.

Gavana pia ameeleza kuwa, katika robo ya nne ya mwaka 2025 ukwasi wa fedha za kigeni ulikuwa wa kutosha, kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya korosho, dhahabu na shughuli za utalii huku urari wa malipo ya nje ukipungua kwa asilimia 2.2 ya pato la Taifa.

Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya Dola 6.3 bilioni za Marekani, kiasi kinachoweza kufanya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi 4.9, ikiwa ni juu ya lengo la angalau miezi 4.

Akiba hii inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, sambamba na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi na kupungua kwa bei za mafuta.

Tathmini ya uhimilivu wa deni kwa mwaka 2024/25 inaonesha kuwa uwiano wa deni la umma kwa Pato la Taifa (kwa thamani ya sasa) ulipungua hadi asilimia 40.6, kutoka asilimia 41.1 mwaka 2023/24, ikiwa chini ya ukomo unaokubalika kimataifa wa asilimia 55.

Katika hatua nyingine, Gavana ameeleza MPC imeamua Riba ya Benki Kuu (CBR) ibaki kuwa asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 ikiwa ni mara tatu mfululizo huku akieleza kuwa, wamezingatia matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa ndani ya lengo la asilimia hadi 5.

Mkutano huo pia umehusisha wawakilishi wa benki nchini, mwakilishi wa Umoja wa Mabenki nchini (TBA) Herman Kasekende amesema sekta hiyo inafurahishwa na ufanisi mzuri wa sekta ya nje na ukuaji wa pato la Taifa vinavyotoa uhakika wa ustawi wa biashara.

Kasekende ametoa pongezi kwa BoT kuwa kuendelea kuimarisha thamani ya shilingi akipongeza mpango wa kuhifadha dhahabu ambao umesema uongeza uhakika na kupunguza mahitaji makubwa ya sarafu ya dola.

 “Benki kuu imekuwa bega kwa bega wakati wa kukosekana kwa ukwasi husuani mwishoni mwa robo ya pili ya mwaka 2025. Tunatarajia zaidi ushirikiano na ubunifu zaidi katika kisimamia sekta hiyo,” amesema Kasekende ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania.