Uamuzi huo umetangazwa Januari 8, 2026 na Gavana wa BoT na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza katika mkutano huo, Gavana Tutuba alisema uamuzi wa kubakiza CBR umefikiwa baada ya tathmini ya kina ya hali ya uchumi wa ndani na wa dunia.
“Uamuzi huu umezingatia matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Kuendelea kubakiza kiwango cha CBR kama kilivyokuwa katika robo ya nne ya mwaka 2025 kutasaidia kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuwezesha uchumi wa taifa kuendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa ndani, Gavana Tutuba alisema uchumi wa Tanzania Bara uliendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha ya takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ikilinganishwa na makadirio ya asilimia 6.
Ukuaji huo ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, madini na ujenzi. Kwa upande wa Zanzibar, alisema uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.
Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba aliwapongeza wadau wa sekta ya fedha kwa jitihada zao zilizopelekea kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu hadi kufikia asilimia 3.1, kiwango kilicho chini ya ukomo unaovumilika wa asilimia 5.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki nchini, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende, aliipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.
Alisema usimamizi huo umechangia kuimarika kwa sekta ya kibenki, kudhibiti mfumuko wa bei, kudumisha utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za kigeni, pamoja na kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni.
