CCM yaibuka kidedea kortini, barua ya Chongolo ikitajwa

Sumbawanga. Ni mgogoro wa umiliki wa ardhi ulioibuka miaka 40 iliyopita lakini sasa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, imewapa ushindi Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kumiliki eneo hilo.

Hii ni baada ya Jaji, Abubakar Mrisha kutoa uamuzi wake Januari 7,2026 katika shauri hilo ambalo barua ya aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye sasa ni Waziri wa Kilimo, ikiwa sehemu ya mabishano kisheria.

Jaji Mrisha katika uamuzi wake, amesema mlalamikaji katika shauri hilo namba 27490 la mwaka 2024, George Ngaiza amefungua shauri hilo ikiwa imepita miaka 40 tangu mgogoro uibuke wakati ukomo wa sheria ni kufungua ndani ya miaka 12.

Ngaiza ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Gerald Ngaiza, alifungua shauri hilo dhidi ya Bodi ya Wadhamini CCM, Kamishna wa Ardhi, Msajili wa Hati na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akidai CCM imepora nyumba yake.

Jaji amesema uamuzi wake huo unafuatia wadaiwa kushindwa kuwasilisha mawasilisho ya maandishi kuhusiana na pingamizi la awali walilokuwa wameliweka hivyo, mahakama ikaamua kulitupa pingamizi hilo la awali.

Hata hivyo, Jaji aliziamuru pande mbili kufanya mawasilisho ya pingamizi mahususi la iwapo shauri hilo limefunguliwa nje ya muda, kabla ya kusikiliza shauri la msingi kwa kuwa hoja hiyo inagusa uwezo wa mahakama kuisikiliza.

Aliyefungua ukurasa wa mabishano ya kisheria ni wakili Anthony Kanyama aliyekuwa akiiwakilisha CCM, ambako katika wasilisho lake, alisema shauri hilo limefunguliwa nje ya muda wa kisheria hivyo linapaswa kutupiliwa mbali.

Wakili huyo alieleza kuwa kwa kuangalia viambatanisho vya shauri hilo, ni wazi vinaonyesha limefunguliwa nje ya muda, akiegemea katika kielelezo ‘Ngaiza 5’, ambacho ni barua ya Chongolo yenye kumbukumbu CMM/U.70.70/20/33.

Katika barua hiyo ya Agosti 3, 2021, Chongolo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, alijibu malalamiko ya Ngaiza ambaye alikuwa analalamikia nyumba yake kuvamiwa na CCM tangu mwaka 1984, ikiwa ni zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Wakili huyo alisema kwa kuzingatia barua hiyo, msingi wa mgogoro huo ni mwaka 1984 na kesi imefunguliwa mwaka 2024 na hivyo kukiuka sheria ya ukomo (law of limitation Act) inayotaka shauri la aina hiyo lifunguliwe ndani ya miaka 12.

Alitoa misimamo ya kisheria iliyotokana na uamuzi mbalimbali wa Mahakama ya Rufani, lakini akaegemea kifungu cha 3(1) cha sheria hiyo ya ukomo na kuomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa kuwa imefunguliwa baada ya miaka 40.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Siyumwe Mubanga aliyekuwa akimwakilisha mdaiwa wa pili (Kamishna wa Ardhi) na mdaiwa wa tatu (Msajili wa Hati), aliunga mkono wasilisho la wakili wa CCM na kusisitiza shauri limefunguliwa nje ya muda.

Alisema kwa maneno yake mwenyewe, ni ushahidi ulio dhahiri kuwa mdaiwa wa kwanza (CCM) anamiliki eneo hilo tangu 1984 na kwamba, mdai alifungua shauri la kwanza 2009 na sasa amefungua shauri lingine ikiwa sasa imepita miaka 40.

“Hii ni kinyume na sheria ya ukomo ambayo inataka mgogoro wa ardhi uwasilishwe katika mahakama ndani ya muda wa miaka miwili,” alisema na kunukuu kifungu cha 3(1) cha sheria hiyo akisema kesi imefunguliwa nje ya muda.

“Njia pekee inayopaswa kufanywa na mahakama kwa shauri lililofunguliwa nje ya miaka 12 ni kwa shauri hilo kutupiliwa mbali,” alieleza na kurejea misimamo mbalimbali ya kesi akisema kwa msingi huo, mahakama haina uwezo kulisikiliza.

Hata hivyo, wakili Mbunga aliyemwakilisha mdai alisema pingamizi kuhusu muda halina mashiko na linapaswa kutupiliwa mbali na kueleza mteja wake alifungua shauri la kwanza mwaka 2009, lakini kuna mambo aliyagundua baadaye.

Alieleza kuwa Agosti 23,2016 aligundua kuwa kiwanja hicho chenye mgogoro kilitolewa kwa njia ya ulaghai kwa mdaiwa wa kwanza (CCM), ambaye baadaye alipata hati ya umiliki kutoka kwa Msajili wa Hati ambaye ni mdaiwa wa pili.

Ni baada ya kugundua hilo, Mahakama Kuu iliiondoa kesi ya awali lakini kwa ruhusa ya kuifungua upya na hilo lipo kwenye kielelezo ‘Ngaiza 6’.

Kuhusu hoja ya ukomo, wakili huyo alisema ingawa kifungu cha 5 cha sheria ya ukomo (LLA) kinasema muda unaanza kuhesabiwa mgogoro unapoibuka, kifungu cha 26 cha sheria kinasema muda huo utaanza pale ulaghai unapobainika.

Wakili huyo alisema mteja wake aligundua ulaghai huo Agosti 3, 2021 na kwamba barua ya Chongolo ambayo wajibu maombi wameigemea, haisababishi muda wa ukomo kwani haifichui madai yoyote ya ulaghai ambayo mdai aliyaeleza.

Alihitimisha kwa kujenga hoja kuwa mashauri ambayo wadaiwa waliyanukuu katika mawasilisho yao hayana maana (irrelevant) kwa sababu hayazungumzii msingi maalumu wa kesi iliyopo mahakamani, hivyo akaomba pingamizi hilo litupwe.

Katika uamuzi wake huo wa Januari 7,2026, Jaji alisema baada ya kusikiliza hoja za kisheria, mawasilisho ya mawakili wa pande mbili na nukuu za kesi mbalimbali, kazi iliyo mbele yake ni kuamua kama kesi imefunguliwa nje ya muda ama la.

Jaji alisema suala la ukomo ni jambo linalokwenda kwenye uwezo wa mahakama kusikiliza na kuamua shauri na kwamba pingamizi hilo la muda limeanzia kwenye wasilisho la mdai mwenyewe (pleadings) hasa barua ile ya Katibu Mkuu wa CCM.

“Barua hiyo inaonyesha mdaiwa wa kwanza (CCM) anadaiwa kuvamia nyumba ya mdai mwaka 1984. Wadaiwa wanasema mdai alifahamu tangu wakati huo kuwa CCM ndio inamiliki lakini sasa imepita miaka 40 ndio amefungua kesi,”alisema.

“Lakini pia wadaiwa wanaendelea kueleza kuwa miaka 15 ilikuwa imepita wakati mdai anafungua kesi ya kwanza mwaka 2009. Kulingana na hoja zao ni kuwa hii yenyewe pia ilikuwa ni kinyume cha sheria ya ukomo,”alieleza Jaji Mrisha.

Lakini Jaji alisema mdai kwa upande wake yeye amewasilisha hoja ya kisheria kuwa muda huo wa ukomo unaanza kuhesabiwa ulaghai unapobainika.

“Nimepitia kwa umakini hoja za pande mbili na hapa naona hoja kuu za kuamua ni mbili. Moja ni kama shauri la mdai limefunguliwa nje ya ukomo na pili ni kama tuhuma za ulaghai inaweza kuokoa shauri lisiangukie sheria ya ukomo,” alisema.

Jaji alisema kwa kutazama maelezo yake mwenyewe aliyowasilisha kortini, ni wazi yanaonyesha anakubali uwepo wa CCM katika eneo hilo ulianza mwaka 1984.

“Wakati mdai anafungua kesi ya kwanza mwaka 2009 tayari miaka 25 ilikuwa imepita wakati ukomo ni miaka 12. Shauri la sasa lililofunguliwa mwaka 2024 ambayo ni baada ya miaka 40 ambayo ni nje zaidi ya muda wa ukomo,”alisema.

Jaji alisema kwa ukweli huo, ni wazi jibu ni kuwa kesi imefunguliwa nje ya muda.

Kuhusu hoja ya pili kama suala la kugunduliwa kwa ulaghai kunaweza kukoa shauri hilo, Jaji alisema anaona hoja hii haina mashiko katika muktadha wa kesi ya kurejesha ardhi ambapo madai ya uvamizi yalijulikana tangu mwaka 1984.

“Ulaghai hausimamishi saa ikiwa mdai kwa kuridhisha angeweza kugundua hali ya ardhi. Kwa maneno mengine, mtu hawezi kutumia ‘ulaghai’ kama kisingizio cha kuchelewesha kesi wakati angeweza kujua ukweli mwenyewe kwa urahisi,” alisema.

Jaji aliongeza kusema,  “kwa sababu zilizotolewa hapa, naona malalamiko ya mlalamikaji kuhusu ulaghai hayana msingi hivyo nalikataa suala hili.”

Kulingana na Jaji, katika shauri hilo, wasilisho la mdai linaonyesha wazi kuwa mdaiwa wa kwanza alichukua umiliki wa eneo hilo mwaka 1984 hivyo dirisha la kisheria la kurejesha eneo hilo ukomo wake ulikuwa ni mwaka 1996.

Jaji alisema kwa mtazamo wake, kufungua shauri hilo mwaka 2024 ni kukiuka waziwazi sheria za nchi na kwamba shauri lililofunguliwa nje ya muda sio dhaifu tu, bali halina sifa hivyo pingamizi la ukomo linakubaliwa na mahakama.