Dodoma. Ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko yakiwamo ya kuhara na kipindupindu, Idara ya Afya ya Jiji la Dodoma imeanzisha kampeni maalumu ya usafi wa mazingira katika mitaa na maeneo ya mikusanyiko ya watu, kwa lengo la kuhakikisha yanakuwa safi na salama kwa afya ya wananchi.
Mbali na hilo, kampeni hiyo pia imelenga kutokomeza mazalia ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama na kufyeka vichaka vilivyopo kwenye makazi ya watu.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Januari 8, 2026, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sebastian Pima amesema kampeni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya idara ya afya, wananchi, viongozi wa masoko pamoja na serikali za mitaa ili kuhakikisha jamii inajilinda dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
Moja ya choo ambacho kimeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete
Amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha ongezeko la uchafu katika maeneo mbalimbali, hali inayochochea kuzaliana kwa nzi wanaosambaza vijidudu vya magonjwa.
“Mvua zimeongeza uchafu ambao ni mazalia ya nzi, hivyo tunawahamasisha wananchi kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi. Nzi hubeba vijidudu kutoka kinyesi na kuvisambaza kwenye vyakula au maeneo mengine, hali inayosababisha magonjwa ya mlipuko,” amesema Dk Pima.
Amesema ili kuua mazalia ya nzi na mbu, kila mwananchi anapaswa kuhakikisha usafi katika maeneo yanayomzunguka, iwe nyumbani au katika eneo la biashara, ili yasivutie wadudu hao hatari.
Pia, amewataka wananchi ambao vyoo vyao vimeharibika au kubomolewa na mvua, kuvirekebisha haraka ili kuepuka kuenea kwa magonjwa ya mlipuko yanayoweza kugharimu maisha ya watu.
Aidha, amewahimiza wahusika wa huduma za majitaka kukagua miundombinu yao ili kuzuia maji hayo kusambaa katika mitaa.
Dk Pima amesisitiza kuwa watu wanaotiririsha majitaka kwenye makorongo na mifereji wanapaswa kuacha mara moja, akieleza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Wafanyabiashara katika soko la Sabasaba wakiwa wamepanga bidhaa zao chini licha ya marufuku iliyotolewa na Idara ya afya ya Jiji la Dodoma. Picha na Rachel Chibwete
Badala yake, amewataka wananchi kushiriki kusafisha mitaro ili kuwezesha maji ya mvua kupita bila kutuama kwenye maeneo ya makazi.
“Tangu mvua zianze kunyesha hatujapata mgonjwa yeyote wa kuhara wala kipindupindu, lakini ni lazima tuchukue tahadhari. Jiji la Dodoma ni njia kuu inayotumiwa na watu kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo yale yenye mlipuko wa kipindupindu, hivyo tahadhari ni muhimu,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Kombo Kombo amesema wafanyabiashara sokoni hapo wameelekezwa kuhakikisha usafi unakuwa kipaumbele kabla ya kuanza kupanga bidhaa zao.
Ameongeza kuwa biashara za kupanga bidhaa chini zimepigwa marufuku kutokana na hali ya matope yanayosababishwa na mvua, ili kulinda afya za walaji.
“Tumesisitiza usafi kabla na baada ya biashara. Ikiwa magonjwa ya mlipuko yatatokea, biashara zitasimama. Pia tumewataka wafanyabiashara wanaofanya kazi karibu na mitaro kuhakikisha haijaziba ili kuzuia maji kutuama na kuwa mazalia ya nzi na mbu,” amesema Kombo.
Naye mfanyabiashara wa chakula katika Soko la Mwembeni, Zubeda Salum, maarufu kama Mama Chai, amesema usafi ni kipaumbele katika biashara ya chakula, akieleza kuwa mazingira machafu huwafukuza wateja na pia huweza kusababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wafanyabiashara.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bwawani uliopo Kata ya Dodoma Makulu, Said Komba amesema elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa ya mlipuko tayari imeanza kutolewa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi na kila mwisho wa mwezi unaendelea kuzingatiwa ili kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa safi na siyo mazalia ya wadudu wanaoeneza magonjwa kama nzi na mbu.
