Dar es Salaam. Ripoti ya utafiti wa ujumuishi wa kifedha wa Finscope ya mwaka 2023 inaeleza kuwa asilimia 47 ya Watanzania wanaoweka akiba zao kupitia njia zisizokuwa rasmi hutunza hela hizo ndani ya nyumba zao.
Hali hiyo inatajwa na wadau wa uchumi kuwa na athari katika uchumi, kwani huondoa kiasi cha pesa kinachopaswa kuwa katika mzunguko, hali inayoweza kufanya nchi kushindwa kufanya makadirio sahihi juu ya ukuaji wake wa uchumi.
Hali hiyo pia inaweza kufanya nchi kuona uchumi wake haukui katika kiwango kinachotakiwa, jambo ambalo ni kinyume na kile kinachoendelea halisi.
Kutunza fedha nyumbani kumekuwa kukisababisha vilio kwa watu pindi inapotokea matatizo, ikiwemo majanga ya nyumba zao kuungua moto.
Matukio hayo yamewahi kuripotiwa kwa nyakati tofauti na vyombo vya habari, huku wengine wakipoteza maisha wakati wakijaribu kurudia fedha zilizokuwa ndani ya nyumba moto unapotokea.
Januari mosi, 2025, moto ambao chanzo chake hakijajulikana uliteketeza vyumba vitatu vya wapangaji katika Mtaa wa Wailesi, Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kusababisha kaya tatu kukosa mahali pa kuishi baada ya moto huo kuteketeza samani na mali zote, ikiwemo fedha taslimu Sh3.4 milioni.
Septemba 17, 2015, nyumba iliyopo Mtaa wa Chama cha Biblia, Kitunda Relini, Wilaya ya Ilala, iliteketea kwa moto sambamba na kuunguza fedha taslimu Sh10 milioni zilizokuwamo ndani.
Si kuteketea kwa hela pekee, bali wakati mwingine kumefanya watu kupoteza maisha. Mfano wake ni mkazi wa Mtaa wa Mwasele, Kata ya Kambarage, mjini Shinyanga, Agness James (33), aliyefariki dunia baada ya kurudi ndani ya nyumba inayoungua kuchukua fedha zake.
Kwanini watu wanatunza hela ndani
Mtaalamu wa uchumi, Dk Eliaza Mkuna, anasema watu wanakuwa na fedha mkononi wakiwa na nia tatu, ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya siku kwa siku, kuchukua tahadhari kwa kuwa hawajui nini kitatokea, na uwekezaji.
Licha ya kuwa na nia nzuri wanapohifadhi fedha hizo ndani ya nyumba zao, Dk Mkuna anasema ni sawa na kuziondoa katika mzunguko rasmi, hasa wa uzalishaji.
“Unapotoa fedha kwenye mzunguko wa fedha ulio rasmi kama benki au mfumo wa kifedha, inakuwa ni upotevu, kwani kuna uwezekano mtu angeweza kukopeshwa kiasi hicho cha fedha, akafanya shughuli zake kama biashara, akalipa kodi na kuajiri watu, lakini anakosa hiyo nafasi,” anasema.
Kinyume chake, kukaa kwa fedha nje ya mfumo kunafanya zisizalishe chochote, pia kunaifanya nchi kuwa katika mahesabu yasiyo sahihi kwani wakati mwingine huweza kuonekana imeshuka kiuchumi au uchumi hauko katika kiwango kinachotakiwa, kumbe ni kwa sababu hela nyingi iko nje ya mzunguko.
“Hali hii inaweza kufanya nchi kushindwa kufanya makisio sahihi kwa ajili ya maendeleo yake,” anasema Dk Mkuna.
Profesa Aurealia Kamuzora anasema fedha ni nyenzo muhimu katika nchi inayowezesha ubadilishanaji wa bidhaa (biashara), mikataba au fedha kwa fedha ili uchumi uweze kukua, hivyo ni muhimu iwe katika mfumo unaotambulika.
“Ingekuwa kama kila mtu angeweka hela ndani, benki zisingekuwepo. Si vizuri kutunza hela ndani, lakini tunafahamu kuwa asilimia kubwa ya Watanzania bado wanatunza fedha ndani,” anasema.
Anasema kuweka fedha benki kuna maana kubwa katika kusisimua uchumi, ambapo mwenye fedha akiweka hela zake benki, basi asiyekuwa nazo atakwenda kukopa, atapeleka fedha hizo katika mradi, atajiri watu na kulipa kodi, huku benki ikipata faida.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka, anasema uchumi unapokwenda mbele, vitu lazima viwe rasmi, na jambo likiwa katika mifumo isiyo rasmi linakuwa changamoto.
“Mtu akifanya kitu katika mifumo rasmi si rahisi kuficha shughuli zake, lakini akifanya vitu na kupata fedha katika njia isiyokuwa sahihi lazima atajificha. Jambo hili linakwamisha mzunguko wa fedha,” amesema.
Anasema ni wakati sasa umefika wa kurasimisha shughuli za kiuchumi ili kujua ni kwa kiwango gani zinafanyika na zitambulike, na kwa kufanya hivyo kutafanya mifumo ya malipo kuwa rahisi.
Anasema vitu vinaporasimishwa, inakuwa rahisi kujua kila kiwango cha fedha kinachoingia kinatoka wapi na kinaelekea wapi, huku akisema malipo ya kidigitali yanaweza kusaidia kufanikisha jambo hilo.
Profesa Kamuzora anasema kuna baadhi ya maeneo ni ngumu kuwashawishi watu kuona kuwa kuweka fedha ndani si jambo zuri, kwani ndiyo kitu walichokizoea, hivyo ametaka suala hilo liangaliwe kwa kina.
“Labda ni waoga wa mfumo, lakini uchunguzi ufanyike ili kubaini nini chanzo kinachofanya watu wengi wakimbie kuweka fedha zao benki na kuona ndani ni sehemu salama,” anasema Profesa Kamuzora.
