BAADA ya jana kupigwa mechi nne za Ligi ya Wanawake (WPL), leo saa 12 jioni itaendelea Simba Queens itakapoikaribisha JKT Queens.
Hiyo sio mechi ya kawaida, bali ni pambano la kisasi kati ya timu hizo mbili ambazo zimekuwa na ushindani mkali.
JKT Queens ambao ni watetezi wa ligi baada ya kutwaa ubingwa wa wanawake msimu uliopita, wanataka kuendeleza ubabe wakati Simba Queens wanapambana kurejesha taji ambalo walilipoteza mbele ya mahasimu wao hao.
Timu hizo msimu uliopita katika ligi Simba iliambulia pointi nne, ikitoka sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani kabla ya kuondoka na ushindi wa mabao 4-3 ugenini katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Hata hivyo, hivi karibuni JKT Queens iliichapa Simba Queens 2–1 katika fainali ya Ngao ya Jamii.
Kwa upande wa Simba ambayo takriban wachezaji wanaoanza ni wapya tofauti na JKT wengi ni waliopo muda mrefu kikosini, imeanza vizuri ikishinda mechi zote sita ikiwemo Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga Princess kwa mabao 2-0.
Mfululizo wa matokeo mazuri kwa Simba ndio unakwenda kuonyesha ugumu wa mechi hiyo kutokana na matokeo ya mabingwa hao kwenye mechi sita wakishinda tano na kutoka sare ya bao 1-1 na Fountain Gate Princess.
Hiyo ni mechi nyingine ya kufungua mlango wa vita ya moja kwa moja kati ya Simba wanaowania ubingwa na JKT Queens wanaopambana kuutetea, na matokeo yake yanaweza kuathiri msimamo wa ligi.
Miongoni mwa wachezaji hatari ambao mabeki wa Simba wanapaswa kuwachunga kwa umakini ni winga machachari, Winifrida Gerald mwenye mabao saba ambaye amekuwa mwiba anapokutana na timu za Kariakoo kwani kama sio kufunga, basi anasababisha faulo.
Mwingine ni mshambuliaji kinda, Jamila Rajabu ingawa hazungumzwi sana lakini mchezaji mwenye madhara makubwa anapopata mpira msimu huu tayari amefunga mabao matatu na kuhusika kwenye mabao matano.
Kwa upande wa Simba, Jentrix Shikangwa bila shaka ndiye mshambuliaji wa kigeni mwenye rekodi nzuri za kuwa na muendelezo wa kufunga, msimu wake wa kwanza 2021/22 aliweka kambani mabao 17 uliofuata nane na msimu jana 23 hadi sasa ana mabao matano.
Mwingine ni Aisha Mnunka wa Simba ambaye msimu uliopita hakufanya vizuri, lakini msimu huu tayari ameweka kambani mabao manne akiwa moja ya nguzo muhimu ya ushambuliaji Msimbazi.
Kocha msaidizi wa Simba, Mussa Mgosi amesema hana presha kukutana na wapinzani wao hao kwani msimu huu kila mechi ni kama fainali.
“Kwa upande wangu sina presha ya kukutana na JKT Queens kwa kuwa ninawafahamu vizuri na wao pia wanatufahamu, hivyo tunapaswa kuingia kwa tahadhari kubwa,” amesema Mgosi, huku kocha wa JKT, Kessy Abdallah akisema ni mechi wanayoichukulia kwa ukubwa akiamini maandalizi waliyoyafanya yatawapa matokeo mazuri.
“Si mchezo wa kudharau, tunapaswa kujituma ili tuweze kupata matokeo mazuri. Tunaomba mashabiki wetu na Watanzania wajitokeze kwa wingi hapo leo,” amesema.
