Katambi Aagiza Kupunguzwa kwa Urasimu katika Huduma za Biashara

Na Pamela Mollel,Arusha 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi, ameiagiza menejimenti ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake kupunguza urasimu usio wa lazima kwa kuimarisha sera, sheria na kuboresha mifumo ya usimamizi wa biashara, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Arusha Januari 8,2026 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha menejimenti ya Wizara kilicholenga kujadili na kufanya tathmini ya utendaji wa Wizara na taasisi zake, kilichofanyika Januari 8, 2026 jijini Arusha, Mhe. Katambi alisema kuwa sekta binafsi si mshindani wa Serikali bali ni mshirika muhimu katika safari ya kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya viwanda na biashara.

Alisisitiza kuwa mifumo na taratibu za udhibiti na usimamizi wa biashara zinapaswa kuwa rahisi, wazi na zenye ufanisi, akibainisha kuwa majadiliano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi ni muhimu ili kuhakikisha sera zinakuwa shirikishi na zenye kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.

Aidha, alisema huduma zinazotolewa kwa wafanyabiashara na wawekezaji zinapaswa kuzingatia uwazi na ushirikishwaji wa sekta binafsi, hususan katika kupendekeza maboresho ya mifumo na marekebisho ya sheria, ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa biashara nchini.

Naibu Waziri Katambi aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, taasisi zake na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi, akisisitiza kuwa sekta binafsi ni mshirika wa Serikali katika kujenga uchumi imara na shindani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, alisema kikao kazi hicho ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya Wizara yanafikiwa, ikiwemo kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, kuongeza ajira, kuwezesha upatikanaji wa mitaji, pamoja na kuhimiza ubunifu na uvumbuzi, ili kuimarisha zaidi sekta ya viwanda nchini.