Njombe. Zaidi ya wananchi 450 kutoka vijiji vya Tarafa za Masasi na Mwambao wilayani Ludewa, wameanza kunufaika na mgao wa kilo 225 za mbegu bora za ufuta zinazotolewa bure na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.
Hii ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wananchi wa ukanda huo kiuchumi na kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Januari 8, 2026 na Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Dk Festo Mkomba wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa mbegu uliofanyika katika Kijiji cha Kipangala, Kata ya Luilo, wilayani humo.
Dk Mkomba amesema mbegu hizo zitapandwa katika ekari 225 na zinatarajiwa kuongeza tija katika kilimo cha ufuta, kukuza uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi mmoja mmoja pamoja na Ludewa kwa ujumla.
Amesema kilo moja ya mbegu ya ufuta inatosha kupandwa katika eka moja na ina uwezo wa kuongeza tija katika kilimo hicho, hivyo kuchangia kuboresha kipato cha wakulima na ustawi wa uchumi kwa wananchi.
Akizungumza kuhusu soko la zao la ufuta, Dk Mkomba amesema ni kubwa na halmashauri inaendelea kushirikiana kwa karibu na wakulima kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika unakuwa rahisi.
Ofisa Tarafa ya Masasi, George Kapongo amewahimiza wananchi kuachana na kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo chenye tija cha kibiashara ili kujikwamua kiuchumi.
“Bei ya ufuta kwa kilo Mei mwaka jana ilikuwa inauzwa kati ya Sh2,900 hadi Sh3,000, kwa maana nyingine, zao hili ni fursa muhimu kwa wakulima kuongeza kipato chao, nawaomba mlichangamkie,” amesema Kapongo.
Naye Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Godfrey Lufome amesema ufuta ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayochangia kupunguza umasikini na kuongeza pato la mwananchi, wilaya na Taifa.
Mmoja wa wananchi walionufaika na mbegu hizo, Nelson Ngonyani ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbegu hizo akisema zao la ufuta litawasaidia kuwa na zao la pili la biashara sambamba na korosho, hatua itakayoongeza kipato chao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Omary Mkangama amewataka wananchi wa maeneo hayo kuchangamkia fursa ya kilimo cha ufuta ili kuongeza uzalishaji, kuinua kipato na kuimarisha uchumi wao.
