Maabara utafiti afya za wanyama yazinduliwa Zanzibar, manufaa yake…

Unguja. Kujengwa maabara ya kisasa ya utafiti wa afya ya wanyama, kutaongeza chachu ya uwekezaji katika sekta ya mifugo. Imeelezwa.

Imeelezwa mara nyingi wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye mifugo walikuwa wakiuliza uwapo wa matibabu ya mifugo kabla ya kuwekeza.

Maabara hiyo imejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Friedrich Loeffler Institute (FLI) ya Ujerumani kwa gharama ya Sh1.2 bilioni.

Hayo yamebainika jana Jumatano Januari 7, 2026 wakati wa uzinduzi wa maabara ya afya ya wanyama katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (Zaliri), Zanzibar ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha sherehe za miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk Salum Soud Hamed amesema hatua hiyo itaongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo.

“Mara nyingi wawekezaji walipokuwa wakitaka kuwekeza kwenye sekta ya mifugo, jambo la kwanza walikuwa wakiuliza kuhusu matibabu ya wanyama, kwa hiyo kujengwa maabara hii kutaongeza chachu ya uwekezaji katika sekta ya mifugo,” amesema Dk Salum.

Mifugo ni moja ya sekta muhimu za kiuchumi kwa wananchi hasa wa vijijini na ni chanzo cha kujipatia kipato na chakula.

Amesema sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita imekuwa ikichangia asilimia 12 ya jumla ya sekta ya kilimo asilimia (24.3) ya pato la Taifa.

“Kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kuongeza uzalishaji na tija pamoja na kuimarisha miundombinu ya uzalishaji,” amesema.

Amesema maabara hiyo siyo tu italeta faida na manufaa kwa wafugaji na wakulima tu, bali pia wadau wa sekta ya misitu hususani kwa upande wa wanyama pori, kwani nao afya zao pia huathirika na maradhi na watahitaji kuchunguzwa na kujua kwa kina aina ya maradhi na vimelea kupitia uchunguzi wa maabara hizi.

Wizara ya Kilimo, inatambua na kuthamini juhudi na mchango uliotolewa kupitia FLI.

  Mkurugenzi wa FLI, Profess Dk Sascha Knauf amesema maabara hiyo yenye miundombinu ya kisasa ni kwa ajili ya binadamu na wanyama na itasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Zaliri, Abdallah Ibrahim Ali amesema kazi za utafiti ni za kujitolea na inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya vifaa na wataalamu kuwa katika hatari ya kupata magonjwa.

Amesema pia kuna changamoto ya wataalamu wachache katika maabara kisiwani humo.

Hata hivyo, amesema katika maabara hiyo iliyozinduliwa, tayari kuna wataalamu watatu wamepelekwa masomoni nchini Ujerumani hivyo watakuja kuongeza nguvu.

Maabara hiyo ya aina yake ni ya mfumo wa makontena na ni ya kwanza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ambayo imeanzishwa na taasisi ya FLI na inategemewa kutoa huduma za kiuchunguzi kwa viwango vya Ujerumani na kimataifa kwa ujumla.

Maabara hii pia itakuwa na mifumo ya Tehama ambayo itawasiliana moja kwa moja na maabara kuu ya FLI ya Ujerumani.

Amesema gharama za mradi huu ni Sh1.2 bilioni kati ya hizo Sh450 milioni zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Sh750 milioni zimetolewa na FLI ya Ujerumani.

Mbali na hayo, pia  FLI tayari wameshawasilisha vifaa vyote  vya kisasa kwa ajili ya maabara ya utafiti wa afya ya wanyama hapa Zanzibar, ikiwemo mfumo wa maabara wa makontena mawili,  Bio-bank mbili kwa ajili ya kuhifadhia sampuli za wanyama kwa muda mrefu.

Vifaa vingine ni jenereta mbili kila moja ikiwa na uwezo wa kilowati 15 na gari moja aina ya Double cabin kwa ajili ya kazi za kukusanya sampuli.

Kupitia SMZ pia imekamilisha ujenzi wa maabara ya microbiology na Parasitology; mabanda ya utafiti wa mbuzi wa nyama, ukumbi wa mkutano, ofisi kwa ajili ya watumishi wa maabara pamoja na vyoo.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema Taasisi imeanzishwa ikiwa na dira ya kuwa na ubora wa kimataifa katika utafiti unaotoa majibu kwa matatizo ya umasikini na uhaba wa chakula nchini.

Ikiwa na lengo kuu la kuchangia katika kukuza uchumi kwa kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na rasilimali za misitu nchini, kwa njia ya utafiti na kubuni teknolojia za kisasa na kuzipeleka kwa wadau.