Dar es Salaam. Wakati wamachinga, mama lishe na waendesha bodaboda nchini wakilalamikia masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameweka bayana kuwa fedha hizo awali zilikuwa zikinufaisha makundi ambayo hayakukusudiwa.
Amesema vikundi vingine vilinufaika na mikopo hiyo licha ya kutokidhi vigezo, huku baadhi yao vikibainika kutofanya shughuli zozote za kiuchumi, hali iliyosababisha fedha hizo kuwanufaisha wasiohusika.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Januari 8, 2026, katika kongamano la mwaka la wamachinga, madereva wa pikipiki na bajaji, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, huku Dk Mwigulu akiwa mgeni rasmi.
Dk Mwigulu amesema Serikali inalichukulia suala hilo kwa uzito na iko tayari kulitatua kwa kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa, wakiwamo wamachinga, mama lishe na madereva wa bodaboda na bajaji.
Awali, baadhi ya wawakilishi wa makundi hayo, akiwamo Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, Ernest Masanja, ameeleza ugumu wanaokumbana nao katika kupata mikopo hiyo, wakidai kuwepo kwa masharti magumu yasiyoendana na mazingira yao ya kazi.
Ameomba Serikali ianzishe benki maalumu ya wamachinga ili mikopo yao ipitie huko badala ya kutegemea benki moja.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Madereva wa Bodaboda na Bajaji, Said Kagomba, amesema awali waliahidiwa na Serikali kuwa mikopo hiyo itakuwa rahisi kupatikana, lakini hali imekuwa tofauti.
Amesema wanapofika benki wanatakiwa kuwasilisha hati za nyumba au wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini na kupokea mishahara kupitia benki husika.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu, amesema Serikali imezipokea changamoto zote na iko tayari kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi za fedha na Wizara ya Fedha.
“Katika suala la mikopo, tumemsikia mwakilishi wa NMB pamoja na mapendekezo ya kuhusisha benki nyingine. Nitakaa na taasisi husika pamoja na Wizara ya Fedha ili kulichakata jambo hili, na baada ya hapo tutatoa taarifa rasmi,” amesema Dk Mwigulu.
Hata hivyo, amesema masharti ya mikopo yanapaswa kuzingatia uhalisia wa walengwa, akisisitiza kuwa si sahihi kwa mama lishe, wamachinga au bodaboda kuhitajika kutoa hati ya nyumba kama dhamana.
“Ukisema fedha hizi zinakwenda kwa bodaboda, mama lishe au wamachinga halafu unaweka sharti la hati ya nyumba, unakuwa umempa kwa mkono mmoja na kumnyang’anya kwa mkono mwingine,” amesema.
Amesisitiza kuwa lengo la mikopo hiyo ni kuyawezesha makundi hayo kiuchumi kwa kuwapatia mikopo nafuu ili waachane na mikopo yenye riba kubwa inayochochea umaskini.
“Hata mke wangu aliwahi kuwa mama lishe, hivyo naelewa changamoto mnazokutana nazo,” amesema.
Amesema lengo la kuanzishwa kwa mikopo hiyo ni jema, lakini utekelezaji wake umeibua changamoto zilizofanya fedha hizo kuwanufaisha wasiokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mama Lishe Taifa, Havijawa Omari, amesema mazingira ya kazi yao yamekuwa kikwazo katika upatikanaji wa mikopo hiyo, akidai hawajawahi kunufaika licha ya kutajwa kama walengwa.
Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu pia amegusia hoja ya makundi hayo kutaka kujulikana yapo chini ya wizara gani, baada ya baadhi yao kudai kutokuwa na wizara moja inayowasimamia kikamilifu.
Wajumbe walitoa maoni tofauti, wengine wakitaka waondolewe Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na kuhamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Vijana au Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wakieleza kuwa wanalipishwa ushuru katika taasisi na maeneo mbalimbali.
Akijibu hoja hizo, Dk Mwigulu amesema Serikali itatoa tamko rasmi baada ya kuyachambua maoni yote yaliyotolewa, akibainisha kuwa kila hoja ina mantiki yake.
“Nilipanga kusema mnahamia wizara gani, lakini baada ya kusikia maoni tofauti nimeona ni busara mjiratibu ili kuyajumuisha. Kuna wanaosema Viwanda na Biashara, kuna wanaosema Wizara ya Vijana, Tamisemi na hata pale mlipo sasa, hoja zote zina mantiki,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali itafanya mabadiliko yanayohitajika ili kuhakikisha makundi hayo yanakuwa chini ya wizara moja itakayowasimamia kikamilifu, akiwataka mawaziri wa wizara husika kuanza kukaa pamoja na kuchambua hoja hizo mara moja.
Aidha, Waziri Mkuu amegusia suala la maeneo ya biashara kwa wamachinga, mama lishe na bodaboda, akisisitiza kuwa kigezo kikuu ni upatikanaji wa wateja.
“Ili biashara zenu ziwe na tija, ni lazima ziwe maeneo yenye wateja. Naelekeza mikoa yote iwashirikishe viongozi wa makundi haya, pale jambo litakapowazidi, walilete serikalini tulichakate na kufanya uamuzi,” amesema.
