Makonda, Katambi wakabidhiwa wizara, Simbachawene atenguliwa

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na utenguzi wa viongozi mbalimbali wa Serikali, akifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, nafasi za Naibu Mawaziri pamoja na uongozi wa taasisi na uwakilishi wa kidiplomasia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 8, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk  Moses Kusiluka katika uteuzi huo, Patrobas Paschal Katambi, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi ya George Simbachawene ambaye ametenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo, Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.

Rais Samia pia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum). Profesa Kabudi kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katika mabadiliko hayo, taarifa imesema Paul Makonda ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nafasi ambayo awali alikuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo.

Aidha, Dennis Londo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, ambapo awali alikuwa  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, huku  Ayoub Mohamed Mahmoud akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika ngazi ya Katibu Mkuu, Rais Samia amemteua Dk Richard Muyungi kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. Dk Muyungi anachukua nafasi ya Mhandisi Cyprian Luhemeja ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Kwa upande wa uteuzi wa mabalozi, Rais Samia amemteua Mhandisi Zena Said,  Waziri Salum ambaye alikuwa katibu wa Rais  pamoja na Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy kuwa Balozi.

Mbali na hao, ameteuliwa Ally Samaje kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), akichukua nafasi ya Dk Mussa  Budeba.

Pia, Rais amemtengua Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Profesa Eliakimu Zahabu.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu  imeeleza uapisho wa viongozi wote walioteuliwa utafanyika  Januari 13, 2026 katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, kuanzia saa 8.00 mchana.