Mambo ya kuzingatia kuendeleza madini ya kimkakati Tanzania

Kwa mujibu wa Ofisi ya taifa ya Takwimu (NBS) Tanzania iliweka rekodi ya mapato ya juu kabisa kutoka katika sekta ya madini mwaka 2024. Mwaka huo mapato ya madini yalifikia zaidi ya Sh2.317 trilioni (takribani dola bilioni 0.9 za Marekani).

Rekodi hii ilifikiwa katika robo ya nne ya 2024. Mapato hayo yaliongezeka kutoka Sh2.283 trilioni yaliyopatikana katika robo ya tatu ya mwaka huo.

Rekodi hiyo iliimarisha nafasi ya Tanzania katika orodha ya nchi zinazotengeneza fedha nyingi kupitia sekta ya madini barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Madini na vyanzo vingine, mafanikio haya yanatokana na mambo kadhaa ikiwemo ongezeko la uzalishaji wa dhahabu. Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa madini hayo barani Afrika, ikitanguliwa na Afrika Kusini, Ghana na Mali.

Rekodi za miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuwa Tanzania inazalisha kati ya tani 40 na 47 za dhahabu kwa mwaka.

Mwaka 2022/23 mauzo ya dhahabu nje yaliingizia nchi kiasi cha dola 2.86 bilioni, na kuwa moja ya bidhaa iliyoingiza fedha nyingi za kigeni.

Sababu nyingine ya kukua kwa mchango wa madini katika pato la taifa ni ukweli kuwa Tanzania ina madini mengi ya aina mbalimbali, yaliyotawanyika katika maeneo mengi.

Takribani aina 40 za madini yanapatikana Tanzania. Hili ni jambo la kipekee sana kwani ni nchi chache sana duniani zimebarikiwa kuwa na aina nyingi za madini kama ilivyo Tanzania.

Ukiacha dhahabu, Tanzania inajivunia kuwa na almasi, makaa ya mawe, shaba na vito vya aina nyingi.

Kwa miaka ya hivi karibuni mauzo ya makaa ya mawe nayo yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la pato la madini. Rekodi zinaonyesha kuwa mauzo ya hayo yamepaa kutoka wastani wa dola 23.2 milioni hadi dola 228.6 milioni kwa mwaka huku mauzo ya almasi nayo yakipanda kutoka wastani wa dola 9.6 milioni hadi dola 66.9 milioni.

Sababu nyingine iliyopaisha mauzo ya madini ni sera nzuri zilizowekwa na serikali kuendesha na kudhibiti sekta ya madini.

Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka sera zinazotoa mwongozo mzuri katika mnyororo wote wa thamani wa madini kuanzia uchimbaji mpaka kuongeza thamani huku suala la ‘local content’ likitiliwa msisitizo mkubwa.

Serikali imeanzisha masoko ya madini katika mikoa yote nchini hadi ngazi ya wilaya katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanakuwa na soko la uhakika wa madini wanayozalisha.

Pamoja na kuongeza kipato kwa wachimbaji hawa wadogo lakini masoko haya yamewapunguzia usumbufu na kuibiwa.

Wakati Tanzania ikijivunia mkusanyiko huo wa madini ambao unalipatia taifa fedha nyingi za kigeni na ajira, utafiti umeonyesha kuwa Tanzania imeingia katika anga mpya za sekta ya madini baada ya kugunduliwa kuwepo kwa kiasi kikubwa cha madini ya kimkakati ambayo hivi sasa ndio gumzo duniani.

Hapo awali ilifahamika kuwa Tanzania ina madini muhimu tu, lakini sasa imeingia kwenye orodha ya nchi zenye hazina kubwa ya madini ya kimkakati pia.

Madini ya kimkakati ni aina ya madini ambayo matumizi yake yanasaidia kutoharibu mazingira, ni tegemezi katika uzalishaji wa nishati safi yna yenye ufanisi mkubwa, yanakuza teknolojia na kuyafanya kuwa mhimili mkubwa wa maendeleo kiteknolojia.

Hapa tunazungumzia madini ambayo yanatumika hivi sasa duniani kwa ajili ya kutengeneza vifaa au bidhaa zisizochafua mazingira kama vile betri za magari yanayotumia umeme, vifaa vinavyotumika kuitengeneza vya vyombo vya anga za mbali, silaha za kisasa, kuzalisha nishati safi na vifaa vya mawasiliano vya kisasa kama kompyuta na simu janja.

Madini kama kinywe, nickel, cobalt, urani na madini adhimu au kwa kimombo rare earth elements (REE) ndiyo yapo katika kundi hili.

Kutokana na umuhimu wake huu, madini haya pia yana ile sifa ya madini muhimu kwani nayo yanainua sana kiuchumi kutokana na mapato. Tena kwa sababu ya mahitaji yake makubwa, madini haya yanaingiza fedha nyingi zaidi.

Wakati dunia ikihangaika kutafuta madini haya kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zilizo rafiki kwa mazingira na kukuza teknolojia, imebainika kuwa Tanzania ni moja ya nchi chache duniani ambayo ina akiba kubwa ya madini ya aina hiyo.

Tanzania ina akiba kubwa sana ya madini haya na kuifanya kushika nafasi ya tatu barani Afrika kwa wingi wa madini hayo na ya nne duniani.

Wataalamu wanasema kuwa madini haya ya kimkakati, iwapo yatatumika vema, yanaweza kuiinua Tanzania kiuchumi kuliko ilivyofanya dhahabu kwa miaka mingi.

Lakini sote tunatambua kile kinachoitwa laana ya rasilimali. Hii inamaanisha kuwa iwapo Tanzania haitakuwa makini, madini haya ya thamani kubwa, ambayo yanahitajika sana duniani, yanaweza kugeuka kuwa laana kwa nchi.

Uzuri ni kuwa mambo haya ya laana ya rasilimali hivi sasa yanafahamika kwa undani na upo uwezekano wa kuikwepa laana hiyo. Inafurahisha kuwa taratibu zilizowekwa na nchi kuhusiana na sekta ya madini, mafuta na gesi, zinalenga, pamoja na mambo mengine, kuiepusha nchi na laana hiyo.

Lakini laana hiyo inakuja kwa njia na namna nyingi. Hivyo sera na sheria zinaweza kuweka kinga kwenye maeneo fulani lakini iwapo litasahaulika eneo moja tu, tunaweza kujikuta katika mazingira ambapo nchi inashindwa kunufaika na madini hayo.

Hivyo, kuna haja kwa serikali kuendelea kushirikisha wadau ili kupata njia anuai muafaka ambazo zinaiwezesha nchi kunufaika na madini hayo.

Mathalani, moja kati ya mambo ambayo yanapewa msukumo hivi sasa ni suala la kuongeza thamani.

Kwa kuwa madini haya mengi hutumika kutengeneza vifaa vya kisasa kama vile betri za magari ya umeme, wadau wanashauri kuwa badala ya kuuza madini ghafi, nchi ihakikishe kuwa inavutia uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini haya.

Ingawa kuwa na viwanda vya aina hii si jambo baya, ni lazima kuzingatia mambo kadhaa ikiwamo upatikanaji wa malighafi nyingine zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zitakazopelekwa sokoni. Kwa mfano, ni kweli kuwa kinywe ndio inatumika zaidi kwenye utengezaji wa betri za magari ya umeme (kwa asilimia 50). Lakini ili kuikamilisha betri hiyo utahitaji pia lithium, nickel, cobalt, manganese, shaba na aluminium pia.

Tanzania inaweza kuwa na hayo madini mengine lakini si yote yameanza kuchimbwa hivi sasa. Hivyo, kama Tanzania ikiamua kuanzisha kiwanda cha kutengeneza betri za magari ya umeme eti tu kwa sababu ina kinywe nyingi, italazimika kuagiza kutoka nje aina nyingine za madini yanayohitajika kukamilisha utengenezaji wa betri hiyo.

Ili kuhakikisha kuwa mambo kama haya yanazingatiwa, serikali imekuwa ikichukua tahadhari kubwa sana. Lakini kwa upande mwingine, tahadhari hiyo imekuwa ikichelewesha uwekezaji katika miradi kuhusiana na madini hayo. Na hilo linaweza kuigharimu nchi kwa namna mbalimbali.

Mathalani, yapo baadhi ya madini yanaweza kurejelezwa kutoka kwenye vifaa ambavyo vimekwisha muda wake. Hii maana yake ni kuwa iwapo Tanzania itaendelea kuchelewa kuwekeza katika kuendeleza madini haya inaweza kufika mahali dunia ikawa inarejeleza madini ambayo tayari yalikwishatumika na vifaa vyake kufikia ukomo. Hii maana yake ni kuwa mahitaji ya madini haya yatashuka na thamani yake pia itashuka. Tanzania ikiendelea kuchelewa kuwekeza kwenye madini ya aina hii inaweza kujikuta ikiwa na hazina ya madini yasiyo na thamani kubwa baada ya miaka michache tu.

Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa soko la madini ya betri linakua kwa kasi isiyokuwa ya kawaida hivi sasa. Hivyo ni vema nchi ikajiunga katika mkondo huu hivi sasa. Lakini hilo halimaanishi kuwa tufanye mambo kwa haraka bila kuzingatia maslahi ya nchi.

Kulingana na makadirio ya Benki ya Dunia, mahitaji ya madini muhimu kwa teknolojia ya nishati safi yataongezeka kwa zaidi ya asilimia 500 ifikapo mwaka 2050. Kwa kinywe pekee, mahitaji ya dunia yanatarajiwa kuongezeka mara nne kufikia 2035, yakichochewa na uzalishaji wa betri za magari ya umeme.