Matumizi ya hundi yaporomoka, malipo kidijitali yakishika hatamu

Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na kupungua kwa kasi ya matumizi ya hundi kama njia ya malipo nchini.

Mabadiliko haya yamechochewa na ukuaji wa teknolojia za kifedha na kuongezeka kwa urahisi wa mifumo ya malipo ya kidijitali, kama vile huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, malipo ya kielektroniki na kadi za benki.

Watumiaji wengi sasa wanapendelea njia hizi mbadala wa taslimu na hundi kwa sababu ni za haraka, usalama na gharama nafuu zaidi kuliko hundi.

Ripoti ya mwaka 2024/2025 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa Katika kipindi husika idadi ya hundi zinazotolewa kwa Shilingi ya Tanzania zilipungua kwa asilimia 18.8 huku thamani yake ikipungua kwa asilimia 8.5.

Hiyo ikiwa na maana kuwa idadi ya hundi zilizotolewa zilishuka hadi kufikia 374,984 huku thamani yake ya jumla ya Sh1.693 trilioni.

 Pia hundi za Dola za Marekani (USD) zilipungua kwa idadi na thamani kwa asilimia 18.87 na 7.30 mtawalia, hadi kufikia hundi 56,366 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 136.40.

 Kwa upande wa hundi za Dola za Marekani kupungua kwake kulitajwa kuchangiwa na ongezeko la matumizi ya Shilingi ya Tanzania katika miamala ya ndani ya nchi.

 Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Eliaza Mkuna amesema zamani matumizi ya hundi yalikuwa ya-naonekana kama njia salama ambayo inamuwezesha mtu kutembea bila kubeba kiwango kikubwa cha fedha.

 Hali hiyo ilifanya watu kuona hundi kama njia rahisi ya kulipia huduma zinazohitaji fedha nyingi kama miradi, mikataba na malipo yoyote yaliyohitaji fedha nyingi.

 “Lakini sasa urahisi wa malipo umehamishiwa katika njia za kielektroniki na kutumia hundi kunaonekana kama njia ili-yopitwa na wakati kwani inahitaji muda mrefu ili uweze kuipata fedha kwa kwenda benki, ipokelewe, ikaguliwe, simu zipigwe ndiyo hela ihamishwe,” anasema Dk Mkuna.

 Anasema suala hili lina athari chanya katika matumizi ya fedha kwani linaongeza ushirikishwaji wa huduma za kifedha ndani ya jamii.

 Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Goodhome Mkaro amesema kushuka kwa matumizi ya hundi maana yake ku-mewekwa miundombinu mizuri ya kidijitali ambayo inawezesha malipo bila kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine, kampuni moja na kampuni nyingine.

 “Watu wamepunguza kwenda benki wakiwa wanataka kulipa wanahamisha tu fedha kwa njia zilizowekwa, hii ime-tokana na kukua kwa uelewa juu ya matumizi ya huduma za kidijitali na imekuwa ni rahisi kutumia,” amesema.

Amesema kupungua kwa matumizi ya hundi ni jambo zuri katika uchumi kwani inawezesha malipo kufanyika kwa haraka huku ikiondoa usumbufu ambao watu walikuwa wakikutana nao awali ikiwemo hundi kukosewa kuandikwa, fedha kugoma (hundi kubounce).

Kukuwa kwa malipo kidijitali

Kuhusu kukua kwa matumizi ya miamala ya kidijitali kunatajwa na Dk Mkaro wakati ambao ripoti hii pia inaonyesha kuwa miamala iliyofanyika kupitia Mfumo wa Malipo ya Haraka Tanzania (TIPS) iliongezeka Katika mwaka wa fedha 2024/25.

Idadi na thamani ya miamala ya kidijitali iliyorekodiwa ilifikia milioni 554.2 zenye thamani ya Sh40.5 trilioni sawa na ongezeko la kila mwaka la asilimia 53 kwa idadi ya miamala na asilimia 98 kwa thamani.

Pia katika kipindi hicho, idadi ya miamala iliyofanyika kwa shilingi za Tanzania kupitia Mfumo wa Uhamishaji Fedha wa Tanzania (TISS) iliongezeka kwa asilimia 3.2 hadi kufikia 4,114,826 (angalia Mchoro 5.1a). Thamani ya miamala hiyo ili-ongezeka kwa asilimia 28.1 hadi shilingi bilioni 340,464.3.

Aidha, idadi na thamani ya miamala iliyofanyika kwa dola za Marekani (USD) pia iliongezeka, hasa kutokana na ulipaji wa madeni ya serikali yanayohusiana na miradi mikubwa ya miundombinu ya umma, uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na miamala ya uhamisho wa fedha.

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Samwel Wangwe amesema kupungua kwa matumizi ya hundi ni ishara kuwa malipo ya kidijitali yameziba pengo lililokuwapo awali jambo analolitafsiri kuwe uelekeo unaostahili.

Anasema malipo yanapofanyika kidijitali yanapunguza muda wa kufanya jambo moja ambalo wakati mwingine ilimlaz-imu mtu kuacha kazi ili aweze kwenda benki kushughulikia hela yake.

“Mimi ni kitabu cha hundi hapa lakini hakitumiki kwa sababu sasa tunalipa kidijitali, ndani ya dakika moja umemaliza kufanya malipo unaendelea na mambo mengine, tunaenda sehemu sahihi,” anasema.

Anasema ujio wa malipo mtandaoni pia unapunguza usumbufu ambao walikuwa wakipata watu awali ikiwemo makosa kidogo katika uandishi yaliyofanya watu kusumbuka na hundi walizonazo.

“Na si hundi tu, hata malipo ya kutumia fedha taslimu yamepungua sana, siku hizi watu wengi wanachagua kulipa kwa kutumia njia nyingine ikiwemo simu au kadi,” anasema Profesa Wangwe.

Anasema ni muhimu sasa kuimarisha usalama zaidi kuimarishwa katika njia za malipo ya kidijitali wakati ambao idadi ya watumiaji wa njia hiyo wanapozidi kuongezeka.

Wakati huduma za malipo kwa kutumia simu yakitajwa katika ripoti hiyo, uchambuzi unaonyesha kuwa ongezeko lina uhusiano na ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa mawakala wa huduma za fedha za simu na ubunifu katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Pia ongezeko hilo linachangiwa na kuwapo kwa kanuni bora na za kisasa zimeongeza imani ya watumiaji, hivyo ku-chochea matumizi zaidi ya mifumo hii.

Huduma za fedha kwa simu zimepanuka zaidi na sasa ni zaidi kutuma na kupokea pesa, zikijumuisha uhamisho wa fedha wa kimataifa na malipo kwa wafanyabiashara.

Matokeo yake, idadi ya watumiaji hai wa huduma za miamala ya simu imefikia milioni 66.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.4 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2023/24. Vivyo hivyo, idadi na thamani ya miamala ya fedha kwa simu imeongezeka kwa asilimia 27.5 na asilimia 27.1, hadi kufikia miamala bilioni 5.670 yenye thamani ya Sh177.107 trilioni.

Kufuatia kuimarika kwa huduma za kidijitali, baadhi ya wafanyabiashara wanafurahi namna ambavyo zimeweka urahisi wa watu kununua bidhaa wakiwa sehemu mbalimbali bila kuwa na ulazima wa kufika sokoni.

“Mambo yamekuwa rahisi, unaweka nguo mtandaoni mteja anaiona na kuulizia ubora wake na ukubwa halafu mnaku-baliana anakutumiaje hela. Hata kama yuko mkoani, nje ya nchi anapata mzigo wake kwa urahisi,” anasema Zubeda Msasanuri.

Maneno yake yanaungwa mkono na Sabrina Mwangi ambaye licha ya kuwa nchini China anaweza kufuatilia uendeshaji wa biashara zake zilizopo Tanzania kwani malipo yote yanafanyika kidijitali.

“Hatupokei fedha taslimu, ukitaka bidhaa unaweka hela kwenye simu tunakutumia ombi la kulipia bidhaa na wewe unaweka namba yako tu ya siri, hii imeweka urahisi katika kufuatilia mauzo na kuondoa mianya ya wizi ambayo watu wamekuwa wakilia kukutana nayo kwenye biashara,” anasema Sabrina.