Muhudumu wa kasino kortini akidaiwa kuiba ‘cheap’ za kuchezea kamari

Dar es Salaam. Muhudumu wa Kasino ya Da Tang, Aisha Kadry (29) amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shtaka la kuiba cheap tatu za kuchezea kamari, zenye thamani ya Sh3 milioni.

Kadry ambaye ni mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani hapo, leo Alhamisi Januari 8, 2026 na kusomewa shtaka lake na karani wa Mahakama hiyo, Aurelia Bahati.

Bahati amedai mbele ya Hakimu Gladness Njau kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 15, 2025 katika kasino ya Da Tang iliyopo mtaa wa Samora na Mirambo, Kata ya Kivukoni wilaya ya Ilala.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa akiwa muhudumu katika kasino hiyo, aliiba cheap tatu za kuchezea kamari zenye thamani ya Sh3 milioni, mali ya Da Tang Cassino Ltd, wakati akijua kitendo hicho ni kosa na kinyume cha sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake alikana na mahakama ilitoa masharti ya dhamana ambayo mshtakiwa alitakiwa kujidhamini kwa kuweka bondi ya Sh3 milioni.

Mshtakiwa alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kuachiwa huru kwa dhamana.

Upelelezi wa kesi haujakamilika na imeahirishwa hadi Januari 21, 2026 kwa kutajwa.