Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Leo XIV, amemteua Askofu Msaidizi Prosper Lyimo aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha, kuwa Askofu wa kwanza na Mwanzilishi wa Jimbo Jipya la Bariadi.
Kuanzishwa kwa jimbo la Bariadi kunafanya idadi ya majimbo ya Kanisa Katoliki kuwa 37 nchini Tanzania, kabla ya hapo yalikuwa 36 ambapo jimbo la mwisho la Bagamoyo lilianzishwa Machi 2025.
Taarifa iliyotolewa leo Januari 8, 2026 na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri John Kitima imeeleza kuwa uteuzi wa askofu Lyimo umeanza leo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mhashamu Askofu Mteule Lyimo alizaliwa Agosti 20, 1964 ambapo baada ya masomo yake ya upadre, alipata daraja takatifu la upadre Julai 4, 1997 jimboni Arusha.
Askofu huyo mteule ambaye kitaaluma ni daktari wa sheria ya Kanisa Katoliki alihudumia katika nafasi mbalimbali na uteuzi huo umemkuta akiwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha alikoanza kuhudumu mwaka 2015.
