Polisi ashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya raia, vifo vitatu vyachunguzwa

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia askari polisi mmoja kwa tuhuma za kumpiga risasi raia, huku likichunguza matukio mengine mawili ya vifo yaliyotokea Rorya mkoani Mara na Arusha.

Taarifa ya kukamatwa kwa askari huyo, imetolewa leo Alhamisi Januari 8, 2026 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kumpiga risasi na kusababishia kifo, Shaban Luluba mkazi wa Nyamwage, Rufiji mkoani Pwani.

Taarifa hiyo inaeleza, askari huyo wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, alifanya tukio hilo, alipokuwa katika ukamataji Januari 8, 2026.

“Uchunguzi unaendelea na endapo itabainika kuna uzembe au matumizi zaidi ya nguvu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari huyo,” amesema.

Mbali na tukio hilo, lingine linalochunguzwa ni kifo cha Dickson Joseph, mkazi wa Rebu Senta Wilayani Tarime mkoani Mara.

Imeeleza kifo hicho kilitokea Januari 1, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime. Baada ya kutokea kifo hicho, Jeshi la Polisi limepokea barua ya malalamiko kuwa, hakikutokana na kijana huyo kuanguka.

Taarifa ya awali ya chanzo cha kifo cha Joseph ilieleza alifariki dunia baada ya kuanguka katika eneo la Mtaa wa Serengeti wakati akikimbia.

Lakini, barua ya malalamiko iliyopelekwa kwa jeshi hilo inadai kifo cha Joseph kimesababishwa na askari Polisi.

“Uchunguzi wa kina umeanza na kulingana na ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia ikibainika kuna askari aliyehusika hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa dhidi yake,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza tukio lingine ni kifo cha Viollete Uwumuhoza, raia wa Rwanda ambaye alijinyonga Januari 7, 2026 akiwa mahabusu ya Polisi jijini Arusha.

Viollete alikuwa katika mahabusu hiyo, akishikiliwa kwa kosa la kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria.

“Uchunguzi wa kina ukihusisha uchunguzi wa kisayansi na wa haraka unaendelea kuhusiana na tukio hilo,” imeeleza taarifa hiyo.