Pwani yajipanga ushindani kimataifa uwekezaji wa viwanda

Kibaha. Mkoa wa Pwani umeanza kuchukua hatua mahsusi za kujipanga kuingia katika ushindani wa kimataifa wa maendeleo ya kiuchumi kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji wa viwanda.

Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika leo Alhamisi Januari 8, 2026 mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema mkoa huo umeanza kujiandaa kushindana kimataifa katika kuvutia wawekezaji kwa kuandaa mazingira rafiki, ikiwemo kupunguza urasimu katika upatikanaji wa ardhi na kuendeleza kongani za viwanda.

Kunenge amesisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa kwa wakati.

Amesema ushindani wa kiuchumi wa sasa unahitaji uamuzi wa pamoja na kasi katika utekelezaji wake.

“Tunapaswa kutambua kuna ushindani wa dunia katika maswala ya uchumi, sasa ili kuwezesha mkoa wetu uongeze nguvu ya uchumi na kuweza kuwahudumia wananchi, lazima tukae na kuweka vipaumbele sambamba na kuandaa mazingira bora ya uwekezaji,” amesema.

Akizungumza katika kikao kazi hicho, Meya wa Mji wa Kibaha, Dk Nicas Mawazo amesema anaamini kuongezeka kwa viwanda mkoani Pwani utakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa wananchi, hasa kwa kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kukuza shughuli za biashara zinazozunguka sekta ya viwanda.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Mwinishee Mlao amewataka madiwani wa mkoa huo kufanya kazi kwa karibu na watendaji wa serikali ili kufanikisha mipango ya maendeleo.

Akizungumza kwa msisitizo, Mlao amesema, “Ukiwa mwenyekiti wa Halmashauri usioneshe uongozi wako nje ya hapo, bali ukiwa nje fanya kama mtu wa kawaida; watu ndio wakuite mwenyekiti.”

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye ongezeko la kasi ya uwekezaji wa viwanda nchini, ukitumia vyema nafasi yake ya kijiografia inayouzunguka Jiji la Dar es Salaam na uwepo wa miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli na bandari kavu.

Katika miaka ya karibuni, mkoa umeendelea kuvutia viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, vinywaji, saruji, dawa na bidhaa za ujenzi, hali iliyochangia ongezeko la ajira, mapato ya Halmashauri na fursa za biashara kwa wananchi wa maeneo ya jirani.

Manufaa ya uwepo wa viwanda Pwani yameonekana kupitia kuimarika kwa kipato cha wananchi, kuongezeka kwa huduma za kijamii, ukuaji wa miji kama Kibaha na Bagamoyo pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta nyingine kama usafirishaji, ujenzi na biashara ndogondogo.

Kwa mkakati unaoendelea wa kuandaa kongani zaidi za viwanda, Mkoa wa Pwani unaonekana kulenga kujijengea nafasi thabiti katika ramani ya ushindani wa kiuchumi wa kitaifa na kimataifa.