Samia: Shirikisheni sekta binafsi kwenye utafiti kupata matokeo chanya

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wahadhiri na watafiti katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zanzibar kushirikiana na sekta binafsi ili tafiti zinazofanyika ziwe na matokeo chanya kwa taifa na wananchi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 8, 2026 wakati akifungua majengo ya IMS Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra ya kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi.

Ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao unatekelezwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ili kuleta mageuzi ya uchumi hususani katika maeneo ya sayansi za bahari. Majengo hayo yamegharimu Sh11 bilioni.

“Niwahimize waadhiri na watafiti katika taasisi hii kushirikiana na sekta binafsi ili tafiti zinazofanyika ziwe na matokeo chanya kwa maendeleo ya nchi na wananchi,” amesme

Pia, ameitaka taasisi hiyo kuanzisha mafunzo mafupi ya vitendo kwa wananchi wanaozunguka katika eneo hilo ambako wengi wanajishghulisha na masula ya uvuvi,  ili kuwaongezea tija na vipato katika kukuza uchumi wa buluu.

Amesema taasisi hiyo ni ya kimkakati Zanzibar kwani imebeba mustakabali wa wananchi na imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wa bahari.

Katika hatua nyingine amewataka wananfunzi wanaosoma na watakaosoma katika taaisisi hiyo, watumie fursa hizo kwa kufanya tafiti na bunifu katika matumizi endelevu ya rasimali za bahari.

“Mtakayoyafanya msiache kuwa waangalifu, ili kuhakikisha rasimali za bahari zinatunzwa na kuendelezwa,” amesema kiongozi huyo wa taifa.

Kwa mujibu wa Rais Samia tafiti katika uchumi wa buluu nguzo muhimu katika kukuza pato la taifa na kupanua ajira kwa taifa huku akibainisha kuwa tafiti zitasaidia katika kukuza sera za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza kuhusu mapinduzi, Rais Samia amesema hayawezi bila kuwa na uwekezaji katika sayansi na tekenolojia kwani ndio msingi katika bunifu na maendeleo ya kweli.

“Majengo haya yanaendana na tafsiri na malengo ya mapinduzi, kwahiyo kukamilika kwake haraka ni matokeo ya uwajibikaji, nidhamu, na uongozi unaoleta matokeo,” amesema Samia.

Ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa ataendelea kuwekeza katika elimu ya juu katika kujenga uchumi shindani, shirikishi na endelevu.

Ametumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia kutoa mchango wake katika kuj3nga sekta ya elimu kutokana na fedha wanazotoa.

Naye Rais mstaafu ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho, Jakaya Kikwete amesema lengo la kuwekeza katika elimu imeendelea kupewa kipaumbele kwa kutekeleza miradi yenye matokeo ya moja kwa moja katika nchi.

Amesema Chuo Kikuu cha Dar es alaam kinaendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunza na kufundishia na pia kinatekeleza tafiti mbalinbali.

Amesema kampasi za Kagera na Lindi nazo zipo katika hatua nzuri na ifikapo Oktoba mwaka huu kamapsi hizo zitaanza kudahili wanafunzi.

Kwa mujibu wa Kikwete, programu ya HEET imeendelea kukifanya UDSM kuwa kinara katika utoaji wa wataalamu katika sekta mbalimbali za kitaaluma.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuomba mambo matatu iwapo wakipata awamu ya pili ya mradi huo au hata isipokuwepo basi Serikali iangalie namna ya kuwasaidia kupitia fedha za serikali.

Ameyataja mambo hayo ni pamoja na kumalizia bweni la wasichana, kuwajengea bweni la wavulana na kuwapatia chombo cha usafiri wa baharini kwa ajili ya kujifunzia.

“Kutokuwa na chombo hicho kunaleta upungufu mkubwa, tunaomba kama mradi huu wa HEET awamu ya pili haya tusaidiwe lakini hata kama hautakuwepp tunaomba serikali iangalie namna inavyoweza kutusaidia,” amesema Kikwete.

Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuwezesha mambo mawili; hati ya eneo hilo na ujenzi wa barabara inayokwenda katika chuo hicho.

Wakati wa kuzindua majengo ya taaluma, utawala na bweni la kike katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Zanzibar.

Waziri wa Elimu Sayansi na Tekenolojia Profesa Adolph Mkenda amesema kupitia mradi huo kuna majengo mbalimbali kama hayo yanaendelelea katika kampasi za chuo hicho kwa mikoa 16 nchi nzima ambapo kuna jumla ya majengo 1177.

Profesa Mkenda amesema katika kuendeleza elimu kuna majengo yanagharimu Dola za Marekani 20 milioni lakini mengine sio ya mradi wa HEET.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye, amesema baada ya kukamilika mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwa wanataaluma kubadilishana uzoefu na kutakuwa na fursa kupokea wataalamu bobezi.

Pia itaimarika kwa tafiti hususani uchumi wa buluu na kutoa suluhisho za changamoto na ubora wa ufundishaji na ufunzaji.

“Kukamilika kwa mradi huu ni hatua mpya ya maendeleo ambapo kutafungua programu mpya sita za bahari ikiwemo shahada ya uvuvi na tekwnolojia ya bahari na shahada ya ufugaji na viumbe majini,” amesema Profesa Anangisye.

Utekelezaji huu unaenda sambamba na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), unaotekelezwa na Serikali kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, kwa lengo la kuboresha mitaala na mazingira ya elimu ya juu ili yaendane na mahitaji ya soko la ajira. Kupitia mradi huu.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimetengewa Dola za Kimarekani milioni 49.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na jengo la taaluma na utawala na bweni la wanafunzi, ulivyovizindua leo, Mheshimiwa Rais.