Unguja. Licha ya sekta binafsi kukuelezwa kukua, imeeleza changamoto ambazo inazipitia za biashara ikiwemo urasimu na gharama kubwa za usajili wa biashara.
Hayo yamebainika jana Jumatano Januari 7, 2025 wakati wa ufunguzi wa Tamasha la 12 la biashara Zanzibar katika viwanja vya maonyesho Nyamanzi Dimani Unguja, ikiwa ni shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Ali Suleiman Amour amesema licha ya sekta binafsi kupiga hatua kubwa Zanzibar, bado kuna changamoto zinazoikabili ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali kukuza mitaji yao na uzalishaji wa pamoja.
Pia amesema kuna tatizo la usajili wa bidhaa katika taasisi husika, gharama kubwa za usajili, urasimu katika usafirishaji bidhaa bado ni kikwazo kwa wafanyabiashara.
Hata hivyo, amesema changamoto hizo isiwe kikwazo na kuwakatisha tamaa badala yake kuwapo na ushirikiano, uwajibikaji, ubunifu na mshikamano katika kushughulikia changamoto hizi.
“Hatua hii inadhihirisha wazi tunapiga hatua za biashara Zanzibar, maana katika maonyesho haya ni jukwaa la wajasiriamali kujifunza, kupanua masoko na kuanzisha biashara mpya, licha ya kuwa bado tuna changamoto zinazoikabili sekta binafsi,” amesema Amour.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Maendeleo ya Biashara Zanzibar, Dk Habiba Hassan Omar amesema maonyesho hayo 12 yanazidi kukua mwaka hadi mwaka tangu yalipoanza mwaka 2014, yakiwa na washiriki 109 mpaka kufikia mwaka huu washiriki ni 316.
“Maonyesho haya yanazidi kukua na kupata mafanikio, washiriki wanaongezeka, kati ya washiriki hao Zanzibar ina washiriki 246, Tanzania Bara washiriki 61 na taasisi tisa kutoka mataifa ya Uganda, Brazil, Congo, Zambia, Burundi na Msumbiji,” amesema Dk Habiba.
Akizungumza wakati akifungua maonesho hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema sekta ya biashara inazidi kuwa tulivu ambapo imesababisha hata mfumuko wa bei kushuka.
Kwa mujibu wa Hemed, mfumuko wa bei umetoka asilimia 6.9 mwaka 2023 na kufikia asilimia 4 mwaka 2025.
“Serikali ya Mapinduzi inaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, majukwaa haya ni muhimu kukuza biashara na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,” amesema Hemed.
Ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi husika kuimarisha mazingira ndani ya taasisi ili kuendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Dk Seleman Hassan Serera amesema Serikali zote mbili zinaendelea kuboresha mazingira ya biashara, hivyo akatumia fursa hiyo kuwaita wafanyabiashara kuendelea kuchangamkia fursa za uwekezaji na kufanya biashara katika pande zote mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrick Ramadhan Soraga amesema waandaaji wanatakiwa kuendelea kuyapa hadhi maonesho hayo kufikia viwango vya kimataifa.
Naye Mkurugenzi wa Unique Touch, ambao wameandaa maonyesho hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Edwin Robert Geo amesema jukumu lao ni kuhakikisha maonyesho hayo yanafikia ngazi za kimataifa hivyo kuiinua Zanzibar kimataifa.
