Dar es Salaam. Wakati Serikali ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo la ajira nchini, sekta isiyo rasmi imeendelea kuwa nguzo ya uchumi kwa vijana wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu nchini.
Serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya elimu, ajira na maendeleo wameendelea kutilia mkazo katika mifumo ya elimu huku kipaumbele cha Serikali kikiwekwa katika uwekezaji wa elimu ya ujuzi na ufundi.
Sekta hiyo imeibuka na kuendelea kuwa tegemeo la mamilioni ya vijana nchini kama njia muhimu na salama ya wasio na ajira rasmi kujipatia riziki kupitia shughuli mbalimbali zikiwemo biashara ndogondogo.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesisitiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ni nguzo muhimu katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi, hususan katika sekta zinazochangia pato la taifa.
Akizungumza Januari 5, 2026, wakati wa ukaguzi wa uendeshaji wa mafunzo ya amali katika Chuo cha Veta cha Njiro, Arusha, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Ameir, amesema elimu ya ujuzi ndio msingi wa kuandaa jamii iliyoelimika, yenye ushindani wa kimataifa na inayochangia maendeleo ya viwanda.
Kuhusu mjadala wa mitaala ya elimu kutokuakisi mahitaji ya soko la ajira ambao umekuwa ukiibuliwa na wadau, Wanu amesema Serikali inaendelea kufanyia maboresho mitaala ya elimu ili kujikita katika elimu ya ujuzi itakayowaandaa wahitimu kukabiliana na changamoto za ajira.
“Maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo yameongeza msisitizo wa elimu ya ujuzi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, ili kuwajenga wanafunzi mapema kuelekea soko la ajira na ujasiriamali,” amesema.
Wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua, sekta binafsi imechomoza ikiongoza uchumi kwa wahitimu, wengi wakiibukia kwenye biashara ndogondogo, kilimo, ubunifu binafsi, uchimbaji mdogo wa madini na fursa zingine zinazopatikana kulingana na mazingira yao kama njia ya kukabiliana na umasikini na kuendesha maisha yao.
Shirika la Kazi Duniani (ILO), linaeleza nchini Tanzania sekta isiyo rasmi inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi na kufanya pia iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa kwa ujumla.
Kutokana na tatizo la ajira katika sekta rasmi, vijana wengi wanapohitimu elimu yao, hukimbilia katika majiji na miji mikubwa na maeneo mengine yaliyochangamka ambako wanaweza kupata fursa ndogondogo za kuwawezesha kujipatia mahitaji yao.
Wanaorudi vijijini wengi hujiajiri katika shughuli zisizo rasmi kama kilimo kidogo, teknolojia za kilimo kama utengenezaji mbolea za asili na uchimbaji mdogo wa madini zikiwasaidia kuchagia upatikanaji wa huduma muhimu kwa familia zao.
Mfanyabiashara mdogo kutoka Urambo Tabora, Enos Bulai anaunga mkono kauli hii akisema sekta binafsi imekuwa mkombozi wa maisha yake tangu alipohitimu elimu ya chuo kikuu miaka sita iliyopita bila kupata ajira rasmi hadi sasa.
“Ujasiriamali ni fursa muhimu ya maisha ambayo kwetu vijana ndiyo tegemeo kuu kwa sababu unapomaliza chuo mtaani hakuna ajira,” amesema.
Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2020, inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya wanaojiajiri katika sekta iasiyo nchini hapa rasmi ni vijana, kundi linalobeba wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu zikiwemo sekondari, vyuo vya kati na wale wa elimu ya juu.
Jumanne Kampalala kutoka Mwanza, kijana aliyeamua kujikita kwenye huduma za ufundi wa kompyuta na kuuza nyimbo kwenye simu anaelezea uhalisia kuhusu ugumu wa kupata ajira, akisema aliamua kujifunza kazi mbalimbali nje ya taaluma yake ya chuoni ili aweze kuendesha maisha yake.
Amesema, tangu alipohitimu chuo kikuu mwaka 2024 akijikita kwenye fani ya ualimu, hajawahi kupata sehemu ya kufanya kazi hivyo akaamua kujiajiri katika sekta isiyo rasmi akifanya kazi ya ufundi wa kompyuta na kurusha nyimbo kwenye simu.
“Tangu nimemaliza chuo kikuu mimi ndoto ya kupata kazi imepotea kabisa na sasa nina ofisi yangu ya kurusha nyimbo huku nafanya na ufundi wa kompyuta kwenye ofisi yangu niliyofungua hapa Mwanza,” amesema.
Mbali nao, wapo vijana wahitimu wa elimu za ngazi mbalimbali wamejiajiri kwenye huduma za bodaboda mijini na vijijini hali inayowawezesha kuendesha maisha yao huku wakiendelea kusaka ajira kwenye sekta rasmi.
Licha ya sekta hii isiyo rasmi kuwa kimbilio la wahitimu wa elimu nchini, wamesema inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinazokwamisha kusonga mbele kama alivyoeleza kiongozi wa chama cha waendesha bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba.
“Huku kwenye bodaboda na bajaji tunao vijana wa ngazi zote za elimu na wapo wasomi waliohitimu vyuo vikuu, kutokana urahisi wa kujiajiri huku wakisubiri fursa za taaluma zao,” amesema Said.
Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusuph amesema wana changamoto za maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao na mikopo yenye masharti magumu na riba kubwa huku wakifanya biashara katika mazingira yasiyo rafiki.
Namoto amesema, pamoja na juhudi mbalimbali za Serikali, vijana wanahitaji kuwekewa mazingira rafiki kibiashara zao ili kuvutia kindi kubwa kujiajiri katika biashara na kupunguza umasikini kwa vijana.
“Kwa sasa vijana wanakopa mikopo ya kausha damu ili kufanya biashara, Mimi ninaona, Serikali ikitenga maeneo mazuri ya biashara zetu na mikopo ya riba nafuu kwa vijana wafanyabiashara ikawepo, vijana wengi watakweza kuvutiwa na kujiajiri,” amesema.
Hata hivyo licha ya magumu hayo, sekta hiyo isiyo rasmi imekuwa kichocheo cha uchumi kwa vijana na kusaidia familia kujikimu, huku ikichangia katika pato la Taifa kupitia kodi mbalimbali na kutoa bidhaa na huduma muhimu kwa jamii.
