Musoma. Serikali inatarajia kuifufua hoteli ya kitalii ya Musoma ambayo imeacha kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 25 sasa, baada ya kutelekezwa na mwekezaji na majengo yake kugeuka magofu.
Hoteli hiyo iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), ni miongoni mwa mashirika ya umma yaliyobinafsishwa kwa watu binafsi kupitia sera ya Taifa ya ubinafsishaji, lakini tangu kipindi hicho haijawahi kufanya kazi, hali iliyosababisha majengo yake kuharibika na kuwa magofu huku ikidaiwa kuwa pango la wahalifu.
Akizungumza baada ya kukagua majengo ya hoteli hiyo yaliyopo eneo la Mwisenge, Manispaa ya Musoma leo Alhamisi Januari 8, 2026, Naibu waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza Juni 2026 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uwekezaji nchini.
“Kwa ufupi ni kwamba mwekezaji tayari amepatikana na wapo katika mazungumzo na TRC kuhusu namna ya kuanza ujenzi na masuala mengine ya uendeshaji, nitumie nafasi hii kumuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha mazungumzo hayo yanakamilika kwa haraka ili ujenzi uanze mara moja,” amesema.
Dk Chaya amesema Serikali hivi sasa imeelekeza nguvu nyingi kwenye sekta ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha na kukuza uchumi wa nchi na watu wake, hivyo inatarajia kutumia fursa zilizopo za uwekezaji kwa ajili ya shughuli hiyo.
Amesema suala la ukosefu wa ajira hususan kwa vijana ni miongoni mwa sababu zilizofanya Serikali kuelekeza nguvu nyingi kwenye uwekezaji ambapo inatarajia kutumia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kutengeneza ajira na kipato kwa Watanzania.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Pius Chaya (mwenye notebook) akiwa katika eneo la Hoteli ya Musoma alipofanya ziara kukagua eneo hilo. Picha na Beldina Nyakeke
Amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali imetumia gharama kubwa katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji na kwamba hali hiyo ilikuwa ikilenga kuiandaa nchi na watu wake kuelekea kwenye uwekezaji endelevu kwa manufaa ya wananchi.
Amesema mbali na hoteli hiyo, pia, tayari Msajili wa Hazina ameanza mazungumzo na wawekezaji wengine wawili kwa ajili ya kufufua kiwanda cha maziwa na cha nguo cha Mutex.
Dk Chaya amewataka Watanzania kubadilisha mtazamo wao kuhusu uwekezaji ambapo amesema Serikali itatumia wawekezaji kutoka ndani na nje kwa ajili ya kufanikisha malengo hayo.
Amesisitiza Serikali haitasita kuwanyang’anya wawekezaji watakaoshindwa kuendeleza maeneo yao na kuwatafuta wawekezaji wengine kwa maelezo kuwa haipo tayari kuona fursa zilizopo zikiendelea kutelekezwa kama ilivyo sasa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema licha ya Serikali ya awamu ya kwanza kujitahidi kujenga viwanda vikubwa mkoani humo kikiwepo kiwanda cha nguo, maziwa na samaki, viwanda hivyo hivi sasa havifanyi kazi.
“Mkoa hauna viwanda kabisa, bahati nzuri fursa zipo nyingi sana, tunahitaji kuwa na viwanda ili tuondokane na kuwa sehemu uzalishaji na usafirishaji wa malighafi na tuweze kuwa wachakataji na kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa zetu,” amesema.
Amesema Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na mambo mengine imejielekeza kwenye uwepo wa viwanda vikubwa vya kati na vidogo, hivyo Mkoa wa Mara, pia, unatakiwa kunufaika na dira hiyo kwani fursa zipo, kinachotakiwa ni uwekezaji.
Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji amesema ufufuaji wa viwanda katika jimbo hilo kutasaidia kuimarisha uchumi wa mkoa na wa mtu mmoja mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema kujengwa kwa hoteli hiyo mbali na kuongeza fursa za ajira na kuimarisha uchumi, pia, kutasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu kwani hivi sasa baadhi ya wahalifu wamekuwa wakitumia magofu hayo kupanga uhalifu.
“Mimi nilikuwa mfanyakazi wa kiwanda cha maziwa na pale kulikuwa na ajira zaidi ya 500, sasa fikiria viwanda vilivyokufa kama cha nguo, samaki na vingine vingi, unaweza kuona namna ajira zilivyokufa na viwanda hivyo,” amesema Musa John, mkazi wa Musoma.
