Serikali kuwakumbuka wasaidizi wa kisheria kwenye bajeti ijayo

Dodoma. Serikali imesema kuanzia bajeti ijayo ya 2026/27, wasaidizi wa kisheria watakuwa kwenye ikama na watatambuliwa na Serikali ili kuimarisha utoaji haki.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Januari 8, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi aliyesema  kada hiyo ilisahaulika lakini wana umuhimu katika kuwafikia watu wa vijijini.

Maswi amebainisha hayo wakati wa hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya wizara yake, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Legal Services Facility (LSF), yanayolenga kuongeza nguvu ya utoaji wa huduma za kisheria nchini.

Amesema Serikali imeona huduma nzuri zinazotolewa na wasaidizi wa kisheria hasa kuyafikia makundi maalumu ikiwemo wazee, akina mama na wenye ulemavu, hivyo lazima itambue mchango huo.

“Muundo wetu katika utoaji haki bado una changamoto hasa kuwafikia watu wa pembezoni ili nao wapate haki, kwa makubaliano haya sasa tunaongeza nguvu na kuanzia bajeti ijayo wasaidizi wa kisheria ambao ni nguzo kubwa tunakwenda kuwatambua kwenye ikama,” amesema Maswi.

Kuhusu namna ya utendaji kazi, amesema makubaliano hayo ni mwendelezo wa mpango wa Samia Legal Aid ambao ulizinduliwa Aprili 20, 2023.

Kwa taarifa zilizorekodiwa, Samia Legal Aid ilifika mikoa yote Bara na Zanzibar ambapo iligusa watu milioni 4.1 wakati migogoro ya ardhi ikichukua sehemu kubwa ya malalamiko, ikifuatiwa na malalamiko ya mirathi na ndoa.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo ameiomba UDOM kufungua ofisi ya mkoa ya kutoa huduma za kisheria ili iwe mfano kwa wengine.

Mkurugenzi wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema makubaliano hayo yamelenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa haki kwani chini ya taasisi yao wapo wasaidizi wa kisheria zaidi ya 4,000 wanaofanya kazi wilayani.

Lulu amesema utendaji kazi wa pamoja unaongeza nguvu na mbinu katika kuwahudumia watu lakini akabainisha kuwa awali walifanya kazi kwa huruma bila kutambulika kisheria.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Lazack Lokina amesema ushirikiano wa kutoa msaada wa kisheria, moja ya faida yake ni kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wanyonge.

Profesa Lokina amesema mbali na mpango huo, bado kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza wataalamu wa sheria watakaowafikia watu wengi vijijini, ambako kuna uhitaji lakini huduma hazifiki.