Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeanza rasmi kupokea maoni ya Rasimu za Kanuni Mpya za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu kwa Madereva za mwaka 2026.
Kanuni hizi zimetayarishwa chini ya Sheria ya LATRA Sura ya 413.
Akifungua Kikao cha Wadau cha Kujadili Rasimu hizo jijini Dar es Salaam tarehe 08 Januari 2026, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, alisema sekta ya usafiri wa abiria na mizigo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi.
“Kuongezeka kwa fursa za usafirishaji kumewezesha sekta binafsi kuwekeza zaidi huku Mwaka 2024, malori 201,388 yalipewa leseni, ikilinganishwa na 183,392 mwaka 2023,” alisema Prof. Kahyarara.
Aliongeza kuwa mabasi pia yameongezeka kwa kiasi kikubwa, ambapo mwaka 2024 mabasi 64,635 ya masafa marefu na mafupi yalipewa leseni, ikilinganishwa na 50,316 mwaka 2023. Hii inaonesha mahitaji makubwa ya huduma za usafiri nchini.
Prof. Kahyarara alisema Serikali imewezesha mabasi ya masafa marefu kufanya safari saa 24, huku akisisitiza matumizi ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa Ufuatiliaji wa Vyombo vya Usafiri (VTS) na i-buttons. Aidha, LATRA App na Safari Tiketi App zinawawezesha abiria kufuatilia mabasi na kulipia nauli kwa urahisi.
Hata hivyo, alibainisha changamoto kubwa ni uchovu wa madereva, unaosababisha ajali na kuhatarisha usalama wa abiria. Kutokana na hili, Rasimu za Kanuni Mpya zinalenga kudhibiti muda wa kazi, mapumziko, muda wa juu wa kuendesha na kubadilishana madereva.
Prof. Kahyarara aliwataka wadau kusoma Rasimu hizo kwa kina na kutoa maoni ili kuongeza ubora na usalama wa usafiri.
Kwa upande wake, Dkt. CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, alisema sekta ya usafirishaji imekua lango kuu la uchumi wa Tanzania kutokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rasimu hizo zinapatikana kwenye tovuti ya LATRA, na maoni yanaweza kutumwa kwa barua pepe au anuani za posta zilizotolewa.








