Shauri la ACT-Wazalendo kupinga ubunge Lindi Mjini lafutwa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara, imefuta shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge Lindi Mjini.

Shauri hilo la uchaguzi namba 30403/2025 lilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge jimboni humo kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Mchinjita Isihaka.

Walalamikiwa katika shauri hilo walikuwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Lindi Mjini (mlalamikiwa wa kwanza), Mohamed Utaly na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi wa kufuta shauri hilo umetolewa leo Alhamisi Januari 8, 2026 na Jaji Said Ding’ohi, baada ya kusikiliza pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo.

Walalamikiwa katika pingamizi hilo walidai shauri hilo halikuwa na nguvu ya kisheria kwa sababu mlalamikaji alishindwa kuwasilisha dhamana ya gharama ndani ya siku 14 kama inavyotakiwa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2025.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Ding’ohi amesema Mahakama inakubali pingamizi hilo, akieleza kasoro iliyobainika haikuwa ndogo, bali kubwa iliyohusisha udanganyifu wa makusudi.

Amesema kwa kuwa shauri hilo halikulipiwa ada bila kibali halali kisheria, analifuta shauri hilo.

Ilidaiwa mahakamani kuwa, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kilimteua wakili Jasper Sabuni kumwakilisha mlalamikaji katika shauri hilo.

Baadaye wakili huyo aliandika barua ya kujiondoa katika shauri hilo akidai aligundua kwamba TLS haikutoa kibali cha kumteua kumwakilisha mlalamikaji.

Mlalamikiwa wa kwanza na wa tatu kupitia wakili wa Serikali waliwasilisha taarifa ya pingamizi la awali, wakidai shauri hilo linakosa nguvu ya kisheria kwa sababu mlalamikaji ameshindwa kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa kwa shauri la uchaguzi kinyume cha kifungu cha 104 (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025.

Walieleza kifungu hicho kikisomwa sambambamba na Kanuni ya 11 (1) ya Kanuni ya Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge, Tangazo la Serikali Namba 431 la Julai 11, 2025, hivyo kuomba Mahakama ifute shauri hilo.

Kabla pingamizi halijaanza kusikilizwa mawakili wa walalamikiwa waliibua hoja mpya wakiomba iangaliwe kwanza, iwapo shauri hilo lipo sawa kisheria, ambao ndiyo msingi wa uamuzi wa jaji.

Mlalamikiwa wa kwanza aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola huku mlalamikaji akiwakilishwa na wakili John Seka.

Kalokola alieleza mlalamikaji alifungua shauri Novemba 23, 2025 na kwa mujibu wa aya ya tatu ya hati ya shauri hili la uchaguzi, alipata msaada wa kisheria kutoka TLS akiaminisha kuwa, wakili Sabuni alipangwa kumwakilisha.

Alidai kutokana na sababu hiyo shauri lilifunguliwa kwa mwamvuli wa mashauri ya msaada wa kisheria, hivyo mlalamikaji akanufaika na matakwa ya kanuni ya 35 (2) ya Kanuni ya Mashauri ya Uchaguzi, Tangazo la Serikali Namba 431/2025, hivyo kutolipa ada ya kufungua shauri kwa msingi kwamba, amepata msaada wa kisheria.

Alieleza kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama Desemba 22, 2025, wakili Sabuni aliitaarifu Mahakama kuwa, amepata taarifa kutoka TLS haitambui maombi hayo na haijawahi kutoa cheti cha msaada wa kisheria kumteua yeye kumwakilisha mlalamikaji katika shauri hilo.

Kwa mazingira hayo, wakili Sabuni aliandika barua kujitoa kumwakilisha mlalamikaji katika shauri hilo.

Kalokola alieleza kitendo hicho kinalifanya shauri kuwa batili kwa kuwa hati ya shauri imebeba uthibitisho wenye uongo, ni shauri lililofunguliwa kwa kukiuka kanuni ya 35 (2) ya Kanuni za Uchaguzi za 2025, kwani limefunguliwa kinyume cha sheria kwa mgongo wa msaada wa kisheria na kwa kuwa mlalamikaji hajawahi kupata msaada huo, angetakiwa kulipa ada ya kufungua shauri kama ambavyo kanuni ya 35 (1) inavyotaka.

Amedai kitendo cha kutolipa ada kinalifanya shauri kuwa batili na nafuu pekee ambayo Mahakama inaweza kutoa ni kulifuta na mlalamikaji alipe gharama.

Mawakili wa mlalamikiwa wa pili waliunga mkono hoja hiyo.

Wakili Seka alieleza mlalamikaji alikuwa akisimamiwa na wakili Sabuni aliyesemekana aliteuliwa na TLS kabla ya wakili huyo kueleza umetenguliwa au hautambuliki, hivyo akalazimika kujiondoa katika shauri.

Seka alikiri ni dhahiri utaratibu wa kisheria ulikiukwa kwa sababu shauri limefunguliwa bila ya kulipiwa ada ya Mahakama.

Hata hivyo, alisema shauri kama hilo haliwezi kufutwa kwa sababu ya kasoro za kutofuatwa taratibu, akaomba Mahakama iione kuwa inaweza kusababisha upotoshaji wa haki.

Seka alisema Mahakama inaweza kuamuru marekebisho ya hati ya shauri kwa mujibu wa kanuni ndogo ya 3 na kuwa kifungu cha 34 kwa jumla, kinalenga kuitaka Mahakama kusikiliza mashauri ya uchaguzi kwa msingi wake, na kama kuna kasoro ndogondogo busara iruhusu kutoa muda wa kurekebishwa.

Alirejea kanuni ya 6 ya Kanuni za Ada za Mahakama ambayo pia inamruhusu mdaiwa kutolipa ada ya shauri la madai mahakamani kwa sababu ya umaskini.

Jaji amesema Mahakama imeangalia kwa makini hati ya shauri, mawasilisho ya pande zote mbili kuhusu pingamizi lililoibuliwa.

Amesema wakili wa mlalamikaji hapingi kwamba shauri lilifunguliwa pasipo kulipiwa ada wala kuweka dhamana ya gharama kwani alilifungua kama mnufaika wa msaada wa kisheria, lakini kiuhalisia hakuwa na kibali cha kufanya hivyo.

“Ni msimamo wa sheria kwamba, shauri la madai litahesabika kwamba limesajiliwa mahakamani iwapo ada stahiki ya Mahakama imelipwa ipasavyo au taratibu za kisheria zimefuatwa kumruhusu mtu ambaye hana uwezo, kutolipa kabisa ada,” amesema.

Amesema katika shauri hilo kama taratibu zingekuwa sawa, mlalamikaji angestahili kunufaika na matakwa ya kanuni ya 35 (2).

Amesema mazingira yanaonesha kabla ya kufungua shauri mlalamikaji alikuwa anafahamu hakuwa na sifa za kunufaika na mwamvuli wa kupata msaada wa kisheria, lakini kwa sababu na namna ambayo yeye anafahamu, alipata nyaraka zilizoiaminisha Mahakama kwamba amepata kibali cha kuanzisha shauri kwa msaada wa kisheria na shauri likafunguliwa kwa kufuata maelezo ya nyaraka hiyo.

Jaji amesema kwa maoni yake ni dhamira ya mlalamikaji kutaka kuipotosha Mahakama.

“Nimemsikia wakili Seka hata hivyo, akisema kwamba mlalamikaji sasa yupo tayari kulipia ada na dhamana ya gharama iwapo Mahakama itakubali kumruhusu kufanya hivyo. Ni vyema nikasema mapema hapa kwamba, sheria haiwezi kuwa rahisi kiasi hicho,” amesema.

“Taratibu zimewekwa ili zitekelezwe kwa manufaa ya kurahisisha utoaji haki, muda wa kufanya hivyo, ulishapita. Wadaawa wanao wajibu wa kufanya matendo mema kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa sheria husika na mara zote katika mchakato wa uendeshaji wa mashauri mahakamani, wanatakiwa watawaliwe na dhamira ya uaminifu na uadilifu.”

Amesema lengo la msingi huo ni kuisaidia Mahakama kutimiza jukumu lake la kutenda haki ipasavyo.

Katika shauri hilo, amesema mlalamikaji hajaweka wazi ni kwa nini alifanya vitendo vya kuipotosha mahakama.

“Kwa hatua ambayo imefikiwa hivi sasa, kwa kweli sioni kama ombi la wakili Seka la kutaka shauri hili lisifutwe bali imruhusu mlalamikaji kufanya marekebisho ya nyaraka za shauri hili linatekelezeka kwa kuwa shauri halijalipiwa ada na halikuwa na kibali cha kufunguliwa kwa mgongo wa msaada wa kisheria, maana yake, shauri lenyewe halipo,” amesema.

“Kwa kuwa shauri halipo, maana yake hakuna nyaraka halali yenye sifa ya kufanyia marekebisho. Ni vyema ikaeleweka kwamba, marekebisho ya nyaraka za Mahakama yanaweza kuruhusiwa tu, kwa nyaraka ambazo zipo mahakamani kihalali tayari, kufuatia maombi ya muhusika wa shauri.”

Amesema kasoro hiyo ni kubwa inayosababisha shauri lisilolipiwa ada bila ya kibali cha mahakama, kuwa batili mbele ya sheria na inasababisha upotoshaji wa haki.

Amekubaliana na mawasilisho ya mawakili wa walalamikiwa akisema: “Nakubaliana na msingi wa maoni yao kwamba, shauri hili ni batili na kimsingi, lilikuwa batili tangu mwanzo. Nafuu pekee iliyopo ni kufutwa kwa shauri hili kwa gharama, kama ambavyo nafanya sasa.”