TMA yatoa tahadhari kwa wavuvi, wananchi waishio mabondeni

Mbeya. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imetoa tahadhari kwa wavuvi na wananchi waishio mabondeni katika kipindi cha msimu wa mvua za wastani na chini ya wastani.

Miongoni mwa tahadhari hizo ni pamoja na uwepo wa mafuriko au makazi kuzingirwa maji kufuatia udongo kushiba kwenye maeneo yenye mikondo ya mifereji ya kutiririsha maji.

Meneja wa TMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elius Lipiki ameliambia Mwananchi leo Alhamisi Januari 7, 2026 wakati akizungumzia utabiri na athari za mabadiliko ya tabianchi katika kipindi hiki.

“Tunatoa tahadhari kwa wavuvi kufuatilia taarifa ya mamlaka husika kutokana na kuwepo kwa hatari ya kupata uoni hafifu, vyombo kupoteza mwelekeo au kupinduka,” amesema.

Lipiki amesema kwa sasa kuna mvua za wastani na chini ya wastani ambazo zimepelekea udongo kushiba maji, lakini kuwepo na mvua chache zinazoweza kuleta madhara kutokana na kasi maji kwenye maeneo yenye mitiririko hususani mito na vijito.

“Utabiri unaonyesha mwisho mwa wiki hii kutakuwa na ongezeko la mvua za wastani ambazo zinaweza kuleta madhara, hivyo tunatoa wito kwa wananchi waishio mabondeni na pembezoni mwa mikondo ya maji na mifereji kuchukua tahadhari na kufuatia taarifa ya TMA,” amesema.

Kuhusu fursa za kiuchumi, Lipiki amesema kipindi hiki cha mvua za wastani na chini ya wastani wakulima wanapaswa kuzitumia kuongeza tija ya kuzalisha na kuchochea fursa za kiuchumi.

Mvuvi katika mwalo wa Matema, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Festo Wille amesema kimsingi wamekuwa na tahadhari kubwa kipindi hiki ambacho kuna mvua kubwa.

“Ni kweli ukiingia majini kuna mawimbi makali na ukungu ambao unafanya washindwe kuona mbali, lakini ambao wanafuatia taarifa za TMA, wanachukua tahadhari ya kuingia majini,” amesema.

Katika hatua nyingine wameomba wataalamu wa TMA kutoa elimu kwa wavuvi katika maeneo ya makambi ili kunusuru maisha yao na vyombo wanavyotumia majini,” amesema.