TPSF yasitisha mkataba wa ajira wa Maganga, sababu yatajwa

Dar es Salaam. Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limetangaza kusitisha mkataba wa ajira na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Raphael Maganga baada ya uchunguzi kufanyika.

Mkataba huo umesitishwa ikiwa imepita miezi mitatu tangu Baraza la Uongozi la TPSF lilipotangaza kumsimamisha kazi Oktoba 3, 2025 na kuagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kiuchunguzi kufuatia kuwapo kwa wasiwasi unaohusiana na masuala ya kiutawala na taratibu za ndani.

Taarifa ya kusitishwa kwa mkataba wa ajira imetolewa leo Januari 8, 2026 na Rais wa TPSF, Angelina Ngalula kwa wanachama, washirika na wadau wa TPSF.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya kukamilika, ripoti ya ukaguzi wa kiuchunguzi ilipitiwa kupitia mifumo ya utawala na nidhamu iliyoainishwa ya shirikisho hilo.

“Kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotokana na mchakato huo, Baraza la Uongozi liliamua kusitisha mkataba wa ajira wa Raphael Maganga kuanzia Desemba 29, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Ili kuhakikisha mwendelezo wa uongozi na shughuli za shirikisho kuendelea bila kukatizwa, Baraza la Uongozi tarehe hiyohiyo lilimteua Deogratius Massawe kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPSF hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.

“TPSF linaendelea kujizatiti katika kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji, uwazi na uadilifu na linaendelea kufanya kazi kwa karibu na wanachama wake, Serikali, washirika wa maendeleo, pamoja na sekta binafsi kwa ujumla ili kuendeleza masilahi ya sekta binafsi nchini Tanzania,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia taarifa hiyo, Maganga amejibu kwa kifupi: “Mimi mwenyewe ndiyo kwanza nimeiona taarifa hiyo, hivyo kwa sasa sina cha kusema labda hapo baadaye.”

Maganga anatoka katika nafasi hiyo baada ya kuhudumu kwa siku 609 tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa TPSF, Februari Mosi, 2024.

Massawe anayechukua nafasi hiyo ni mchumi, mtaalamu wa fedha na sera akiwa na shahada ya uzamili ya biashara katika uhasibu, shahada ya kwanza ya forodha na usimamizi wa kodi, diploma ya kitaaluma katika viwango vya kimataifa vya uhasibu wa sekta ya umma (IPSAS).

Pia, Massawe ni Mhasibu wa umma aliyesajiliwa (CPA) na mkufunzi wa fedha aliyeidhinishwa na  (CFE), anachukua nafasi hiyo akiwa na uzoefu katika sekta ya ushauri kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi na aliwahi kuhudumu kama mkuu wa idara ya fedha wa TPSF.