Musoma. Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, imewasili mkoani Mara ambako itakutana na makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo waathirika wa vurugu zilizotokea wakati huo.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Chande Othman, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kubaini sababu za kilichotokea wakati wa uchaguzi huku ikipewa miezi mitatu kukamilisha kazi hiyo.
Akizungumza baada ya kuwasili mjini Musoma leo Januari 8, 2026, Kamishna wa Tume hiyo, Balozi Radhia Msuya amesema hivi sasa wajumbe wa Tume hiyo wamegawanyika katika makundi matatu kwa ajili ya kutembelea mikoa iliyopata kadhia hiyo.
Katika Mkoa wa Mara, amesema wajumbe wawili wanatarajiwa kukutana na walengwa kwa muda wa siku tatu kuanzia leo ili kuwasikiliza.
“Tumepewa siku 90 kufanya hii kazi, sasa baada ya kumaliza pale Dar es salaam tumejigawa makundi matatu kwa ajili ya kufika kwenye mikoa hasa ile iliyopata kadhia hii na Mkoa wa Mara ni miongoni mwa iliyoathirika,” amesema.
Kamishna wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio yaliyotokea Oktoba 29,2025, Balozi Radhia Msuya akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi baada ya wajumbe wa tume hiyo kufika mkoani Mara kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. Picha na Beldina Nyakeke
Amesema pamoja na mambo mengine, Tume hiyo inatarajia kuwa na majibu ya namna gani nchi imefikia hali hiyo na kwa namna gani inaweza kujinasua kwenye hali hiyo ambayo amesema Tanzania haikuwa na kawaida ya kuona mambo kama yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na wajumbe hao, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Kanali Mtambi amewapongeza kwa kufika mkoani humo na kuwaomba kutekeleza majukumu yao kwa uhuru bila woga wowote.
Kanali Mtambi amesema kukamilisha jukumu lao kwa weledi kutalisaidia Taifa kupata suluhu ya yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa mwaka 2025 kwa kuwa mamlaka husika itafanyia kazi matokeo ya Tume ili hali kama hiyo isijirudie.
“Sasa tumefikaje hapa na yaliyojiri ni yapi na tunatokaje hapo, kila mtu anawasubiri mtuambie tunatokaje kwa sababu hatutaki yajirudie, sisi wana Mara tuna matumaini na Tume,” amesema Kanali Mtambi.
Balozi Msuya ameongozana na mjumbe mwenzake, Balozi David Kapaya na kwa pamoja leo wanatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa kabla ya kwenda wilayani Tarime na Bunda ambako watakutana na makundi mbalimbali ya wanajamii.
Makundi yanayotarajiwa kukutana na ujumbe huo wa Tume ni pamoja na bodaboda, mama lishe, watu waliopoteza mali zao, majeruhi na ndugu wa watu waliopoteza maisha kutokana na vurugu hizo.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wameiomba Tume hiyo kutenda haki kwa kuhakikisha maoni yao yanafanyiwa kazi, huku wakitoa wito pia kwa walengwa kujitokeza ili kutoa maoni yao kwa Tume hiyo.
“Hakuna mtu aliyependa kushuhudia hali kama ile, tunaomba tu hii Tume iwe huru kabisa, ikusanye taarifa kwa weledi na kuzifikisha kunakohusika ili zifanyiwe kazi ipasavyo,” amesema Sadiki Rajabu.
Kwa upande wake, Josiah Kitundu amesema itakuwa na ajabu endapo Serikali itaamua kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kuwafikia walengwa kupitia Tume hiyo na mwisho wa siku maoni ya wananchi yasifanyiwe kazi.
