Arusha/Dar. Wanasheria wawili wa Tanzania, Tito Magoti na Bob Wangwe wameishtaki Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), wakilalamikia ukiukwaji wa taratibu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Magoti na Wangwe wamefungua shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Katika shauri hilo la Rejea namba 59/2025, Magoti na Wangwe wanapinga mchakato na matokeo ya uchaguzi huo ambao pamoja na mambo mengine, wakidai haukukidhi viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia na kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Pia, wanadai uchaguzi huo ulikuwa ni wa hadaa, kwa misingi ya uvunjifu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Mkataba wa EAC).
Wamebainisha vifungu wanavyodai vilikiukwa ni pamoja na kifungu cha 6(d), wakidai uchaguzi huo na matukio yake havikuzingatia misingi ya utawala bora, demokrasia, utawala wa sheria, pamoja na haki za binadamu na za watu.
Kingine ni kifungu cha 7(2), wakidai vitendo vya mamlaka kabla, wakati na baada ya uchaguzi vilikosa uwazi, uadilifu na kuheshimu haki za kisiasa, kinyume na kanuni shirikishi za uendeshaji wa EAC.
Vilevile wametaja kifungu cha 8(1) (c), wakidai usimamizi wa uchaguzi huo na hatua za baadaye za dola vilidhoofisha demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, na hivyo kuhatarisha malengo na utekelezaji wa mkataba.
Vifungu vingine vya Mkataba wa EAC wanavyodai vimekiukwa ni pamoja na 27 (1), 28, 29, 30 (1) na Kanuni ya 1 na 25 za Kanuni za Utaratibu wa Mahakama ya Afrika Mashariki.
Kufuatia ukiukwaji huo, wanasheria hao wanaiomba mahakama itamke kuwa vitendo vya uzembe wa Tanzania vinavyohusiana na uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 vimekiuka Mkataba wa EAC.
Pia wanaiomba itamke kuwa mchakato wa uchaguzi huo na matokeo yake yaliyotangazwa Novemba mosi, 2025 havikutimiza viwango vya lazima vya uchaguzi wa kidemokrasia chini ya sheria na miongozo iliyokubaliwa ndani ya EAC, AU na SADC.
Vilevile wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uvunjifu mkubwa wa haki kabla, wakati na baada ya uchaguzi ulifanya mchakato huo kuwa siyo uchaguzi, kinyume na Mkataba wa EAC na kanuni za kidemokrasia.
Kisha wanaiomba mahakama hiyo iamuru uchaguzi huo ulikuwa na kasoro za msingi na hivyo ni batili chini ya viwango vya EAC.
Pia wanaiomba mahakama hiyo iamuru uchaguzi mpya ufanyike kwa kuzingatia Mkataba na kanuni za uchaguzi za EAC na viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia vya AU na SADC.
Mbali na amri za kubatilisha uchaguzi huo, pia wanaiomba mahakama iiamuru Tanzania ilipe fidia, malipo ya madhara kwa waathirika pamoja na kuchukua hatua za urekebishaji stahiki, ikijumuisha huduma za kitabibu, kisaikolojia, kisheria na kijamii kwa waathirika na jamaa zao.
Katika kesi hiyo, Magoti na Wangwe wanawakilishwa na Mawakili Arnold Tsunga, Donald Deya, Jeremiah Bamu na Jebra Kambole.
Akizungumza na Mwananchi kwa leo Alhamisi Januari 8, 2026, Wangwe amesema chini ya Mkataba wa EAC, Tanzania ina wajibu wa kuzingatia kanuni za msingi za EAC.
Amefafanua kuwa ukiukwaji wa Mkataba wa EAC wanaoulalamikia, unajumuisha, utawala bora ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni za demokrasia, utawala wa sheria, haki ya kijamii, fursa sawa, uwajibikaji na uwazi.
Shauri hilo linasubiriwa kupangwa kwa ajili ya usikilizwaji katika kikao kijacho cha Mahakama ya EACJ.
Hii ni kesi pili kufunguliwa katika mahakama hiyo kuhusu uchaguzo huo, baada ya ile ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inayohusu kitendo cha kuzima mtandao kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025.
Kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2025, iilifunguliwa na mawakili wa LHRC wakiongozwa na Jebra Kambole na Peter Majanjara.
Katika shauri hilo, LHRC inadai Oktoba 29, 2025 majira ya saa tano asubuhi, mtandao ulizimwa, hataua ambayo iliathiri Tanzania nzima kwa kipindi hicho.
LHRC inaeleza kuwa, kuzimwa kwa mtandao kuliathiri Watanzania kiuchumi na kijamii kwa kuwakosesha fursa ya kupata taarifa za msingi kwa njia ya kidijitali kama kutumia benki ya mtandaoni, kupata huduma za afya mtandaoni, na kuwanyima mawasiliano na hivyo kuathiri uchumi kwa kuleta hasara ya mamilioni ya shilingi.
LHRC inaiomba mahakama itoe tamko kwamba kuzimwa kwa mtandao kumeiuka vifungu 6(d), 7(2), 8(1) (c) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia, itamke kwamba kuzimwa kwa mtandao kulileta athari kubwa kwa umma, iizuie Tanzania isirudie tena kuzima mtandao bila kuwa na sheria ya kuiruhusu kufanya hivyo au bila kuwa na amri ya mahakama.
