Hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa rasmi Kanuni mpya za uendeshaji wa shughuli za kibenki zi-nazozingatia misingi inayoepuka riba. Kanuni hizi zitahusu uendeshaji benki zinazoepuka riba, na pia benki za kawaida zinazokusudia kutoa huduma za kifedha kupitia madirisha maalum yanayojulikana kama Islamic win-dows.
Kutolewa kwa kanuni hizi ni hatua ya kihistoria katika sekta ya fedha nchini, kwani zinaweka mfumo mahsusi wa kisheria unaoratibu uendeshaji wa benki zinazotoa huduma kwa mtindo huo mbadala ambao utasaidia kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika huduma rasmi za kifedha nchini.
Moja ya masuala muhimu ndani ya kanuni hizi ni ulazima wa kutenganisha fedha za wateja wa huduma za Kiislamu kutoka katika fedha za shughuli za benki ya kawaida. Kwa mujibu wa mwongozo huo mpya, benki au taasisi ya fedha itakayochagua kuendesha huduma kwa mtindo huu itatakiwa kutoa ahadi iliyoandikwa ya kuhakikisha kuwa fedha na akaunti za biashara ya benki isiyo ya riba zinatunzwa tofauti kabisa na zile za benki ya kawaida.
Vilevile, taasisi hizo zitalazimika kuwa na vitabu vya hesabu na kumbukumbu tofauti kwa ajili ya uendeshaji wa huduma hizo. Utaratibu huu kitaalamu (ring-fencing), unaweka uzio wa kiutendaji unaozuia kutangamana kwa fedha ndani ya benki inayotoa huduma kwa mitindo yote miwili kwa pamoja (commingling of funds).
Kwa mtazamo wangu Sharti hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu kadhaa za msingi;
Kwanza, ikiwa fedha zitachanganywa na mifumo ya kawaida ya kibenki, uhalali wa kifiqhi wa miamala yote ya benki hiyo unakuwa na shaka. Shariah ya Kiislamu katika masuala ya fedha haisisitizi tu ustadi wa kuandaa mi-kataba na huduma za kibenki, bali pia huzingatia kwa makini asili ya fedha zinazotumika na namna zi-navyoelekezwa katika miamala.
Mathalan, benki inaweza kubuni bidhaa na kuzitaja kuwa ni Shariah-compliant. Hata hivyo, iwapo fedha zilizo-kusanywa kupitia amana za wateja wa huduma za Kiislamu zitachanganywa na fedha nyingine zisizo katika mtindo huo, huduma hizo hupoteza msingi wake wa kisheria na kimaadili.
Vilevile, kwa upande wa amana, deposits za wateja wa dirisha la Kiislamu zinapochanganywa na amana zi-nazotokana na shughuli za kawaida za kibenki, hutokea kupotea kwa utambulisho wa kiutendaji wa benki ya Kiislamu na kuvurugika kwa misingi iliyotumika kama nguzo ya huduma za fedha zisizo na riba. Hivyo, itatia shaka mantiki nzima ya mfumo wa benki ya Kiislamu hata kama bidhaa zake zitaendelea kutangazwa kuwa zinafuata Shariah.
Pili, kutenganisha shughuli hizi kimahesabu na katika mtindo wa ndani wa uendeshaji kunasaidia kuepuka changamoto za kiuendeshaji na kurahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa kibenki. Hii ni kwa sababu mfumo wa utoaji huduma za fedha za Kiislamu hufungamanisha miamala yake na mali halisi (asset-based financing), au uwekezaji kwa mtindo wa kugawana mapato na hatari (risk sharing), jambo ambalo ni tofauti kabisa na utaratibu wa benki za kawaida.
Kwa mfano, huduma za kifedha kama Murabaha, Musharakah au Mudarabah zinahitaji utaratibu maalum wa hesabu, udhibiti na usimamizi wa hatari. Kutenganisha fedha na vitabu vya hesabu kunafanya benki kui-marisha ukaguzi huru wa ndani, kudhibiti utekelezaji wa kanuni za Shariah, na kurahisisha ufuatiliaji wa shughuli za benki kwa upande wa wasimamizi na wateja.
Tatu, kuna uwezekano kwamba benki inaweza kupata mapato yasiyoendana na Shariah kwa bahati mbaya. Ukizingatia kuwa mfumo mzima wa kibenki wa Kiislamu bado unafanya kazi ndani ya mazingira ya mfumo wa kawaida. Endapo kutakuwa na utaratibu madhubuti wa kutenga hesabu na fedha za dirisha la Kiislamu, itaku-wa rahisi kwa benki kugundua mapato hayo ambayo kisharia yatalazimika kutolewa kwa hisani. Utaratibu huu utasaidia kujua kwa uwazi ni fedha zipi ni safi na zipi zinahitaji kutakaswa kuepuka mapato yasiyokubalika kisharia.
Nne, utaratibu wa kutenganisha fedha na akaunti za benki isiyo na riba ni nyenzo muhimu ya kuongeza imani ya wateja katika uendeshaji wa benki za Kiislamu. Hadi sasa, sehemu ya wananchi wenye dhamiri ya imani imeendelea kuwa na shaka ikiwa taasisi hizi ni kweli zinaepuka riba kikamilifu. Utenganishaji katika kuendesha shughuli hizo ni mbinu nzuri kukuza Imani ya watumiaji huduma za kibenki.