Vaibu la mapokezi ya Taifa Stars

KULIKUWA na vaibu la aina yake jana wakati wa tukio la kuwasili kwa kikosi cha Taifa Stars kilichorejea kikitokea nchini Morocco lilikoenda kushiriki Fainali za 35 za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zilizofanyika nchini humo.

Timu hiyo iliandika historia mpya katika soka la Tanzania kwa kufuzu hatua ya 16-Bora kwa mara ya kwanza, kabla ya kuaga mashindano hayo kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Morocco katika mechi iliyogubikwa na uamuzi tata wa marefa.

Kutambua mafanikio hayo ya kihistoria, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliandaa safari maalumu ya ndege kuwarejesha nchini wachezaji na maofisa wa timu, hatua iliyopokewa kwa shukrani kubwa kutoka kwa timu pamoja na mashabiki.

Mapema tu asubuhi kuanzia saa 3:20 asubuhi mashabiki walianza kufurika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘Terminal 3’ kwa ajili ya kuipokea timu hiyo.

STAR 01

Mashabiki hao wakiwamo wale wa Yanga, Simba, Azam na wengine walikutana uwanjani hapo wakiwa wote na nguo za jezi ya timu ya taifa wakicheza muziki na burudani nyingine wakiisubiri Stars.

Saa 6:28 mchana Ndege ya Shirika la Tanzania aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliwasili Uwanja wa Ndege ikiwa na kikosi cha Taifa Stars kisha msafara huo kutoka nje saa 6:47 mchana na kupokewa na viongozi mbalimbali wakiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu wake, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya Albert Msando (Ubungo), Dalmia Mikaya (Kigamboni) na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oscar Milambo na maofisa wengine wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), akiwamo Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (NSC), Neema Msitha.

STAR 02

Kiungo mshambuliaji wa Stars Simon Msuva mara baada ya kuwasili, amesema licha ya kufikia hatua ya 16-Bora na kutolewa na wenyeji Morocco kwa kupoteza kwa bao 1-0, wamejifunza mengi tayari kwa fainali zijazo zitakazofanyika kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Tanzania, Uganda na Kenya.

Msuva akizungumzia mchezo wa mwisho dhidi ya Morocco alilia na waamuzi wa mechi akisema waliwanyonga katika matukio mengi ingawa wanaheshimu uamuzi wao.

“Ukiniuliza mimi nitakwambia walituonea, kuna maeneo mengi, lakini imeshatokea na uamuzi wa waamuzi wa soka ndio wa mwisho ila tumejifunza mengi, tutakapokuwa wenyeji tutafanya kitu kikubwa,” amesema Msuva.

“Tunawashukuru sana Watanzania wote ambao wamekuwa wakiiombea mema nchi yetu na hata hawa ambao wamekuja kutupokea hiki ni kitu kikubwa kwetu, tunawashukuru pia serikali kwa yote makubwa iliyotufanyia nisiwasahau TFF.”

STAR 03

Akizungumza uwanjani hapo Kabudi amesema baada ya hatua hiyo Rais Samia amewapa mwaliko maalum Stars, ambapo atakutana nao Januari 10 pamoja na wanamichezo wengine waliofanya vizuri.

“Tanzania inajivunia hii timu kwa namna ilivyoipa heshima nchi yetu, tulikuwa na malengo ya kushinda mechi moja, lakini ndani yake ilikuwa ili twende 16-Bora na ikatimia licha ya kupata sare mbili,” amesema Kabudi.

“Hii ni dalili kwamba Fainali zIjazo tutafanya makubwa zaidi, tuendelee kudumisha amani na Rais atakutana na wachezaji hawa Januari 10, ili akawapongeze na wanamichezo wengine.”

STAR 04

Wakati Msigwa akimkaribisha kocha wa muda wa Stars, Miguel Gamondi, aliwahoji mashabiki uwanjani hapo kama wanataka Muargentina huyo apewe timu ya taifa au arudi Singida.

Mashabiki hao wakalipuka kwa nguvu wakisema kocha huyo apewe kibarua hicho cha kuifundisha Stars huku wakipinga kurudishwa katika klabu yake ya Singida BS.

STAR 05

Baada ya Salam hizo msafara wa Stars ulianza safari ukiwa kwenye basi maalum lililonogeshwa kwa picha za wachezaji wa timu hiyo, uliopita Buguruni. Ilala na kwenda posta ilipo hoteli ya Tiffany ambayo timu hiyo imefikia.