Shinyanga. Katika mkutano wa hadhara unaohusisha usikilizwaji wa kero za wananchi katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, wananchi wamelalamikia kelele zinazofanywa na waendesha bodaboda, jambo linaloleta mshtuko na taharuki.
Wakizungumza leo Januari 8, 2026 katika mkutano uliofanyika viwanja vya Zimamoto, wananchi hao wameeleza kuwa kelele hizo zimekuwa kero kwa sababu zinaleta mshtuko na kuhatarisha afya za wananchi hasa wenye presha.
Mfanyabiashara wa mapambo ya ndani, Anastazia Kulwa ameeleza: “Kuna sauti kubwa zinazotoka kwenye pikipiki kama milipuko, zinatoka mfululizo wakiwa wanaendesha bodaboda. Zimekuwa kero jamani, hadi mapigo ya moyo yanaenda kasi, zinashtua sana, watatuua na presha,” amesema.
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zimamoto Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Kwa upande wake, muuza duka la rejareja soko la Nguzo Nane, Aneth John amesema: “Kila mtu ana matatizo yake, wengine wana presha, milio hiyo kwa namna ilivyo ya kushtua, ikisikika inahatarisha afya, tunaomba viongozi angalieni namna ya kuzuia hili kwa haraka kuepuka madhara.”
Naye mkazi wa kata ya Mjini, Iddi Shabani amesisitiza kuwa: “Licha kelele kubwa wanazozifanya waendesha bodaboda, pia, huendesha kwa mwendokasi bila tahadhari, ajali nyingi zimetokea,” amesema.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi katika viwanja vya Zimamoto mkoani humo.
Akizungumzia kero hiyo, Mtatiro ameagiza kufanyika kwa msako wa kuwakamatwa waendesha bodaboda waliotoboa eksozi za pikipiki zao na kutishia afya na usalama wa wananchi, hususan wenye presha.
Watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hizo, pia, kelele ni uchafuzi wa mazingira,” amesema Mtatiro.
Pia, ameongeza kuwa, “Viongozi wa sasa ni kukaa na jamii, kupata ushauri, maoni na kusikiliza kero zao mbalimbali na kuzitatua kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, pia, wananchi tuwe mbele kulinda amani yetu.”
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zimamoto Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Katika hatua nyingine, Mtatiro amewakumbusha wananchi siku ya kufungua shule ni Januari 13, 2026, watoto wote wenye sifa ya kupelekwa shule wapelekwe, na hataki kuanza kukimbizana na mzazi yoyote.
