Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema maendeleo ya elimu kwa mtoto sio jukumu la mwalimu pekee, hivyo wazazi wanapaswa kuwasimamia watoto kila hatua kupata haki yao ya elimu.
Amesema ushirikiano baina ya wazazi na walimu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio ya watoto, endapo wazazi na walezi watakuwa tayari kuwasimamia wakiwa nyumbani, hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.
Dk Saada amebainisha hayo leo Alhamisi Januari 7, 2026 katika hafla ya ufunguzi wa Skuli ya Msingi Potoa ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Serikali imeshafanya jukumu lake la kutengeneza miundombinu ya skuli na vifaa, hivyo kilichobaki ni wazazi na walezi kuwasimamia watoto wafikie mafanikio ya elimu,” amesema waziri huyo.
Pia, Dk Saada amewataka wazazi kuhudhuria vikao vinavyoandaliwa na walimu skuli kwani vinatoa mustakabali wa wanafunzi, hivyo waache tabia ya kutohudhuria vikao hivyo.
Vilevile, amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii kwani kabla ya Mapinduzi wazee walikosa haki yao ya elimu jambo ambalo lilisababisha umaskini wa maarifa.
Amesema Mapinduzi ya fikra ni matumaini ya kuleta mageuzi nchini kwenye sekta mbalimbali na kurahisisha utendaji kazi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Amos John amesema skuli hizo zimegharimu Sh6 bilioni.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Rashid Simai Msaraka amesema uboreshaji wa sekta ya elimu ni kuifanya kuwa imara ili baadaye wayalinde Mapinduzi kwa kutumia elimu na sio kwa mapanga.
Ameeleza kuwa majengo hayo yanaendana na matokeo kwani ufaulu unaongezeka kwa kiasi kikubwa.
