Anayedaiwa kujipatia fedha za ‘kijiko’ kuendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Mfanyabiashara na raia wa India, Dharmendra Gaikwad (49) anayekabiliwa na mashtaka ya kujipatia  sita yakiwemo ya kujipatia Sh457 milioni kwa njia ya udanganyifu, ataendelea kusota rumande hadi Januari 22, 2026 kutoka na upelelezi kesi hiyo kutokukamilika.

Gaikwad anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa madai kuwa angemuuzia Hezron Kamali, lori aina ya Tipa na  Excavator (kijiko) ambayo ni mitambo ya inayotumika katika ujenzi wa barabara, migodini na bandarini.

Mbali na Gaikwad, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Kampuni ya Al- Zahria Tanzania Limited.

Wakili wa Serikali Titus Aron ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Januari 9, 2026 mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati kesi hiyo ilipotajwa.

“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii bado unaendelea hivyo tunaomba mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi umekamilika” amedai Wakili Titus.

Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza taarifa hiyo aliahirisha kesi hadi Januari 22, 2026 kwa ajili ya kutajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Gaikwad alidai kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, tukio analodaiwa kulitenda Februari 28, 2025 eneo la Vingunguti, ambapo alijipatia Sh82milioni kutoka kwa Hezron Kamali, kwa madai kuwa atamnunulia Excavator, wakati akijua sio kweli.

Februari 14, 2025 mshtakiwa huyo alijipatia Sh40milioni kutoka kwa Kamali kwa madai kuwa atamuuzia Excavator.

Shtaka la tatu, Julai 2, 2025 eneo la Vingunguti kwa lengo la kudanganya, mshtakiwa alijipatia Sh200mil kutoka kwa Kamali,  kwa madai kuwa atamuuzia Kamali Excavator, wakati akijua sio kweli.

Vilevile mshtakiwa alijipatia Sh73milioni kutoka kwa Kamali kwa madai kuwa atamuuzia lori aina ya Tipa, wakati akijua kuwa ni uongo.

Vilevile, mshtakiwa huyo pamoja na kampuni hiyo, walijipatia Sh62 milioni kutoka kwa mlalamikaji kwa madai kuwa wangemuuzia mtambo wa Excavator.

Shtaka la sita ni kutakatisha fedha, ambapo kati ya 28 Machi  na Julai 2, 2025 eneo la Vingunguti lililopo wilaya ya Ilala, mshtakiwa alijipatia jumla ya Sh457milioni kupitia akaunti ya benki ya ABSA yenye jina la Al Zahrin Tanzania Limited, wakati akijua ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia pesa kwa udanganyifu.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alifikishwa Mahakamani hapo Desemba 30, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.