Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mkazi wa Ocean Road jijini Dar es Salaam, Sajjad Dawoodbhai (79) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matatu yakiwamo ya kughushi hati ya umiliki wa ardhi na kuwasilisha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dawoodbhai amefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa Januari 9, 2026 na kusomewa kesi ya jinai namba 528 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali, Titus Aron mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Akimsomea mashtaka yake, wakili Titus amedai mshtakiwa anadaiwa kati ya Desemba 1, 1998 na Desemba 3, 1998 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es salaam, kwa nia ya kudanganya, alighushi uhamisho wa umiliki wa hati ya kiwanja namba 28676, ikidaiwa kuonyesha kwamba Taiyabali Dawoodbhai alisaini, wakati akijua ni uongo.
Shtaka la pili pia ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Desemba Mosi na 3, 1998 Jijini Dar es salaam, kwa nia ya kudanganya, alighushi uhamisho wa haki ya umiliki wa hati ya kiwanja nambari 28676, ikidaiwa kuonyesha kwamba yeye ni mmoja wa Wakurugenzi wa Tanzania Glass Works Limited, wakati akijua kuwa sio kweli.
Shtaka la tatu ni kutoa hati ya uongo, ambapo kati ya Januari Mosi, 1999 na Februari 10, 1999 ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alitoa hati ya uongo kwa udanganyifu, yaani uhamisho wa haki ya umiliki wa hati kiwanja namba 28676 kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Tanzania, wakati akijua nyaraka hiyo ni ya uongo.
Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake amekana kutenda na upande wa mashtaka umesema upelelezi umekamilika hivyo wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali.
Mshtakiwa kupitia wakili wake, Augustino Kusalika ameomba apewe dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili linadhaminika.
Hakimu Nyaki amekubaliana na ombi la mshtakiwa na kutoa masharti mawili, ambayo ni mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria wenye barua kutoka Serikali ya Mtaa watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
Pia, mshtakiwa hatakiwi kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama.
Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo amerudishwa rumande hadi Januari 22, 2026.
